WANASAYANSI WA MABADILIKO YA HALI YA HEWA NA TABIANCHI DUNIANI WAKUTANA ARUSHA
WANASAYANSI WA MABADILIKO YA HALI YA HEWA NA TABIANCHI DUNIANI WAKUTANA ARUSHA
WANASAYANSI WA MABADILIKO YA HALI YA HEWA NA TABIANCHI DUNIANI WAKUTANA ARUSHA
Arusha, Tanzania | 2 Novemba 2026
“Kwa Tanzania kuwa mwenyeji wa mkutano huu ni ishara ya dhamira yetu ya kuimarisha ushirikiano wa kimataifa na kutumia sayansi katika kujenga mendeleo endelevu. Mabadiliko ya hali ya hewa na tabianchi si tishio la siku zijazo pekee athari zake tayari zinaonekana duniani kote hasa katika nchi zinazoendelea zikiwemo nchi za Afrika na nchi za visiwa vidogo” alisema Waziri wa Uchukuzi, Mhe. Prof. Makame Mnyaa Mbarawa (MB), wakati akiwasilisha hotuba ya ufunguzi kwa niaba ya Waziri Mkuu wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Dkt. Mwigulu Lameck Nchemba (MB), katika ufunguzi wa Mkutano wa Tatu Wa Wataalamu wa Jopo la Kimataifa la Sayansi ya Mabadiliko Ya Hali ya Hewa na Tabianchi (IPCC) jijini Arusha.
Mhe. Mbarawa alisisitiza umuhimu wa kutumia taarifa za kisayansi za mabadiliko ya hali ya hewa na tabianchi katika mipango na uwekezaji wa muda mrefu. Alieleza kuwa miundombinu na shughuli za sekta kama ya uchukuzi hukabiliwa na athari za mvua kubwa, mafuriko, joto kali, dhoruba na matukio mengine ya hali mbaya ya hewa.
Naye, Dkt. Ladislaus Chang’a, Mkurugenzi Mkuu wa Mamlaka ya Hali ya Hewa Tanzania (TMA) na Makamu Mwenyekiti wa IPCC, alieleza kuwa huduma za hali ya hewa na hususani tahadhari za mapema za matukio ya hali mbaya ya hewa ni muhimu sana katika kukabiliana na athari za mabadiliko ya hali ya hewa na tabianchi na zinahitaji ushirikiano wa pamoja baina ya sekta, jamii na wanasayansi.
Kwa upande wake Mwenyekiti wa IPCC, Prof. Sir Jim Skea, aliipongeza Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mkoa wa Arusha na Mamlaka ya Hali ya Hewa Tanzania (TMA) kwa mchango na ushirikiano wao katika kufanikisha mkutano huo.
Aidha, alisisitiza umuhimu wa matumizi ya lugha sahihi na yenye kuzingatia unyeti wa kisera katika mawasilisho ya kisayansi ya IPCC, akieleza kuwa waandishi wanapaswa kuchagua maneno kwa umakini ili kuhakikisha taarifa zinabaki kuwa sahihi kisayansi, zinaaminika na zinakuwa na mchango mkubwa katika michakato ya maamuzi na sera za kukabiliana na mabadiliko ya hali ya hewa na tabianchi.
Mkutano huo unafanyika kuanzia tarehe 2 hadi 6 Novemba 2026 katika Kituo cha Mikutano cha Kimataifa cha PAPU jijini Arusha. Unawakutanisha Wataalamu bingwa wa sayansi ya mabadiliko ya hali ya hewa na tabianchi duniani kutoka nchi 75, kwa lengo la kuimarisha mchango wa Kikosi Kazi Namba 1 cha Jopo la Kimataifa la Sayansi ya Mabadiliko ya hali ya hewa na Tabianchi katika kuandaa Tathmini ya Saba ya IPCC kuhusu Mabadiliko ya Hali ya Hewa na Tabianchi.
Mkutano huu umeandaliwa na IPCC kwa kushirikiana na Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kupitia TMA unatoa fursa ya kuimarisha ushirikiano kati ya wanasayansi wa Tanzania, Afrika na wa kimataifa, pamoja na kuongeza ushiriki wa Afrika katika mchakato wa IPCC.

