TMA YAWEKA WAZI MAFANIKIO NA MCHANGO WAKE KATIKA SEKTA ZA UCHUKUZI NA UJENZI
TMA YAWEKA WAZI MAFANIKIO NA MCHANGO WAKE KATIKA SEKTA ZA UCHUKUZI NA UJENZI
TMA YAWEKA WAZI MAFANIKIO NA MCHANGO WAKE KATIKA SEKTA ZA UCHUKUZI NA UJENZI
Mwanza, 16 Novemba 2026
Mamlaka ya Hali ya Hewa Tanzania (TMA) imeshiriki katika Mkutano wa 19 wa Tathmini ya Maendeleo na mikakati ya Sekta ya Uchukuzi, unaofanyika katika Hoteli ya Malaika jijini Mwanza kuanzia tarehe 16 hadi 18 Novemba 2026. TMA imeeleza mafanikio na mchango wake katika kuimarisha sekta za uchukuzi na ujenzi nchini.
Mkutano huo umefunguliwa na Waziri Mkuu wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Dkt. Mwigulu Lameck Nchemba (MB), ukiwakutanisha wadau mbalimbali wa sekta ya uchukuzi na ujenzi kwa lengo la kupitia utekelezaji wa mipango, mafanikio, changamoto na kuweka mikakati ya kuendeleza sekta hizo.
Katika mkutano huo, TMA imetumia fursa hiyo kueleza mchango wake katika kutoa huduma za hali ya hewa zinazosaidia kupanga, kusimamia na kutekeleza shughuli mbalimbali za uchukuzi na ujenzi. Huduma hizo ni muhimu katika kuimarisha usalama, ufanisi na ustahimilivu wa miundombinu dhidi ya athari za hali mbaya ya hewa na changamoto za mabadiliko ya hali ya hewa.
Akizungumza katika mkutano huo, Mkurugenzi Mkuu wa TMA na Makamu Mwenyekiti wa Jopo la Kimataifa la Sayansi ya Mabadiliko ya Hali ya Hewa na Tabianchi, Dkt. Ladislaus Chang’a alieleza mafanikio yaliyopatikana na mchango wa TMA katika kuhakikisha taarifa na huduma za hali ya hewa zinawafikia wadau wa sekta ya uchukuzi na ujenzi kwa wakati ili kuwawezesha kufanya maamuzi sahihi.
Sambamba na wasilisho hilo, TMA imeshiriki katika maonesho yanayoambatana na mkutano huo kupitia banda lake, ambapo washiriki na wadau mbalimbali wamepata fursa ya kujifunza kuhusu huduma zinazotolewa na Mamlaka, teknolojia zinazotumika pamoja na mchango wa taarifa za hali ya hewa katika shughuli za maendeleo ya nchi.
Kupitia maonesho hayo, TMA inaendelea kusisitiza umuhimu wa matumizi ya taarifa za hali ya hewa katika kupanga na kutekeleza miradi inayotekelezwa na nchi kwa ujumla wake sambamba na kulinda miundombinu ya usafiri.

