Historia & Majukumu
Mamlaka ya Hali ya Hewa Tanzania (TMA) ilianzishwa kwa sheria ya Mamlaka ya Hali ya Hewa Na.2 ya mwaka 2019, kupitia Tangazo la Serikali GN 459 la Tarehe 14 Juni 2019. Ikiwa na jukumu la kuratibu, kudhibiti na kutoa huduma za hali ya hewa katika Jamhuri ya Muungano wa Tanzania.
Mamlaka hii inatokana na uliokuwa wakala wa hali ya hewa Tanzania ulionzishwa kwa sheria ya wakala (Executive Agency Act) sura Na. 245 marejeo ya Mwaka 2022. Kabla ya wakala wa hali ya hewa, huduma za hali ya hewa nchini zilikuwa zinatolewa na iliyokuwa idara ya hali ya hewa nchini (Directorate of Meteorology) ambayo ilianzishwa Mwaka 1977 baada ya kuvunjika kwa iliyo kuwa jumuiya ya Africa Mashariki, iklwa na jukumu la kufanya uangazi na kutoa taarifa za hali ya hewa nchini.Kabla ya Jumuiya ya Africa Mashariki huduma za hali ya hewa nchini zilitolewa chini ya Taasisi ya hali ya hewa iliyokuwa chini ya wakoloni.
Aidha, Mamlaka inamiliki Chuo cha Taifa cha Hali ya Hewa kilichopo mkoani Kigoma(www.nmtc.ac.tz).
Majukumu ya Mamlaka ya Hali ya Hewa Tanzania:
- Kudhibiti na kuratibu shughuli za hali ya hewa nchini;
- Kuangaza, kukusanya, kuchakata, kuhifadhi data na kusambaza taarifa za hali ya hewa;
- Kuanzisha na kuendesha mtandao wa vituo vya hali ya hewa vya nchi kavu, kwenye maji na anga ya juu ambao ni muhimu kwa ajili ya kupata taarifa za hali ya hewa;
- Kutoa huduma za hali ya hewa kwa ajili ya usalama wa maisha na mali kwa watumiaji mbalimbali wa huduma za hali ya hewa;
- Kutoa tahadhari dhidi ya matukio ya hali mbaya ya hewa na kuhakikisha kunakuwa na Mamlaka moja yenye kutoa tahadhari za matukio ya hali mbaya ya hewa;
- Kuandaa na kutoa taarifa juu ya klaimatolojia, hali ya klaimatolojia na tafsiri mbalimbali zinazohusiana na masuala ya hali ya hewa;
- Kushirikiana na taasisi na mamlaka nyingine katika masuala yanayohusiana na hali ya hewa ikiwemo mafunzo, tafiti, mazingira na katika masuala ya hali ya hewa na yale yanayohusiana na mabadiliko hali ya hewa;
- Kukusanya mapato yanayotokana na data na huduma nyingine mahususi za hali ya hewa;
- Kutoa huduma za hali ya hewa kwa wadau wa sekta ya maji ikiwemo usafiri wa kwenye maji, uvuvi na shughuli nyingine zinazofanyika kwenye maji;
- Kutoa huduma za hali ya hewa kwa sekta ya usafiri wa anga, tahadhari na taarifa nyingine kwa ajili ya usafiri wa anga kulingana na mahitaji ya Kikanda na Kimataifa;
- Kushirikiana na taasisi nyingine za kitaifa na kimataifa kuhusiana na masuala ya utafutaji na uokoaji unaohusiana na usafiri wa anga na wa kwenye maji;
- Kuhifadhi data zote za hali ya hewa nchini;
- Kuhakiki na kutengeneza vifaa vya hali ya hewa kwa ajili ya matumizi ya ndani na ya nje;
- Kuhakikisha viwango vya kimataifa na miongozo ya utoaji wa huduma za hali ya hewa ikiwemo ya ufungaji wa vifaa vya hali ya hewa inazingatiwa;
- Kufanya tafiti, kutoa elimu na mafunzo ya hali ya hewa pamoja na klaimatolojia na masuala yanayohusiana nayo, kufanya uchambuzi wa data za hali ya hewa kwa ajili ya matumizi ya mipango ya maendeleo;
- Kusajili na kudhibiti vituo vya hali ya hewa;
- Kushiriki katika shughuli za mashirika ya kimataifa zinazohusiana na masuala ya hali ya hewa; na
- Kutekeleza majukumu mengine kulingana na maelekezo ya Mheshimiwa Waziri.

