WADAU SEKTA YA HALI YA HEWA WAJADILI UTABIRI WA MASIKA 2026
WADAU SEKTA YA HALI YA HEWA WAJADILI UTABIRI WA MASIKA 2026
Dodoma, tarehe 2 Februari 2026:
Wadau kutoka sekta mbalimbali nchini wamekutana kujadili utabiri wa msimu wa Masika 2026 na kutoa ushauri wa kisekta katika Mkutano wa 25 wa Wadau wa Sekta ya Hali ya Hewa katika msimu wa Masika uliofanyika tarehe 2/2/2026, Jijini Dodoma. Mkutano huo ni mwendelezo wa ushirikishwaji wa wadau katika utoaji wa taarifa za hali ya hewa kwa ajili ya maendeleo ya kiuchumi na kijamii nchini.
Mgeni Rasmi kwenye mkutano huo, Mh. Jaji Mshibe Ali Bakari ambaye ni Mwenyekiti wa Bodi ya TMA alisema “msimu wa Vuli mwaka 2025 ulitawaliwa na vipindi virefu vya ukavu katika maeneo mengi ya nchi, usahihi wa utabiri ulikuwa kwa asilimia 94.1, ikiwa ni kiwango kikubwa sana, natoa wito kwa wananchi waendelee kuiamini TMA, wazingatie taarifa zinazotolewa na kuzitumia katika shughuli zao za kila siku".
Aidha, alisisitiza kuwa majadiliano ya mvua za Masika kwa mwaka 2026, yazingatie kwa kina athari zinazoweza kujitokeza pamoja na kutoa ushauri wa hatua stahiki za kuchukua kwa ajili ya matumizi ya taarifa hizo katika sekta mbalimbali zinazochangia ukuaji wa uchumi.
Awali, akimkaribisha Mgeni Rasmi, Mkurugenzi Mkuu wa TMA na Makamu Mwenyekiti wa Jopo la Kimataifa la Sayansi ya Mabadiliko ya Hali ya Hewa na Tabianchi, Dkt. Ladislaus Changa, alisema "katika kupunguza pengo la uelewa wa tahadhari za hali ya hewa, Mamlaka imeendelea na juhudi za kushirikisha wadau, katika kuandaa taarifa zinazolenga kuchochea matumizi sahihi ya huduma za hali ya hewa nchini"
Dkt. Changa aliongeza kuwa TMA imeendelea kufanya shughuli zake kwa ubora unaoendana na viwango vya kitaifa na kimataifa na kuifanya Tanzania kuwa moja ya nchi zinazoaminika kwa utoaji wa huduma bora za hali ya hewa duniani. Kupitia viwango hivyo,Tanzania imechaguliwa kuandaa Mkutano wa Nne wa Kimataifa wa Watalaam Bingwa wa Hali ya Hewa Duniani, mwezi Juni 2026.
Kwa upande wa wadau, walitoa pongezi na shukrani kwa TMA kwa ushirikiano wanaoendelea kupata katika kuwasilisha taarifa za hali ya hewa kwa jamii. "Naipongeza TMA kwa kuandaa mkutano huu wa wadau wa hali ya hewa.Sisi ili tuweze kufanya kazi zetu ni lazima tupate taarifa zinazotusaidia katika mipango yetu ya kazi ili kulinda usalama wa wananchi na mali zao".Alisema Kaimu Mkurugenzi wa Kamisheni Ya Maafa, Ofisi ya Makamu wa Rais wa Pili wa Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar, Ndg. Muhidin Ali Muhidin
Mamlaka inatarajia kutoa utabiri wa msimu wa Masika 2026, tarehe 5/2/2026.

