TMA YAANDAA MAFUNZO YA KUIMARISHA UKUSANYAJI, UCHAMBUZI NA USAMBAZAJI WA TAKWIMU ZA HALI YA HEWA
TMA YAANDAA MAFUNZO YA KUIMARISHA UKUSANYAJI, UCHAMBUZI NA USAMBAZAJI WA TAKWIMU ZA HALI YA HEWA
TMA YAANDAA MAFUNZO YA KUIMARISHA UKUSANYAJI, UCHAMBUZI NA USAMBAZAJI WA TAKWIMU ZA HALI YA HEWA
Dodoma ,Tarehe 19/01/2026.
Mamlaka ya Hali ya Hewa Tanzania (TMA), kupitia Mradi wa Climate Risk and Early Warning Systems (CREWS), inaendelea kuimarisha huduma za hali ya hewa nchini kwa kuandaa mafunzo maalum kwa wataalamu wake yanayolenga kuongeza uwezo wa kitaalamu katika ukusanyaji, uchambuzi na usambazaji wa takwimu za hali ya hewa kwa ajili ya kuboresha huduma za tahadhari za mapema.
Katika ufunguzi wa mafunzo hayo, Dkt. Ladislaus Chang'a, Mkurugenzi Mkuu wa Mamlaka ya Hali ya Hewa Tanzania (TMA) na Makamu Mwenyekiti wa Jopo la Mabadiliko ya Hali ya Hewa na Tabianchi (IPCC), alishukuru Shirika la Hali ya Hewa Duniani (WMO) kwa ufadhili wake kupitia Mradi wa CREWS uliowezesha kufanyika kwa mafunzo haya.
Akielezea zaidi, Dkt. Chang’a alisema kuwa mafunzo hayo ni sehemu ya mkakati wa kuimarisha ubora wa huduma za hali ya hewa pamoja na utoaji wa tahadhari za mapema kwa wadau mbalimbali. Aliwahimiza wakufunzi wa mafunzo hayo kuhakikisha wanatumia vyema fursa na maarifa watakayopata katika kuimarisha huduma na kuwa chachu ya kuongeza umahiri na ufanisi katika utekelezaji wa majukumu ya kila siku. Aidha, alisisitiza umuhimu wa kuimarisha uwajibikaji, kufanya kazi kwa bidii na uzalendo, na kutaka kila mtumishi wa TMA kuwa na msukumo wa maendeleo kwa wengine na Taifa kwa ujumla.
Aidha Bi. Mecklina Merchades, Kaimu Meneja wa Kitengo cha Hali ya Hewa Kilimo, alieleza kuwa mafunzo hayo ni matokeo ya kikao kilichofanyika mwezi Agosti 2025, kilicholenga kuainisha mahitaji ya kitaalamu kwa wataalamu wa TMA ili kuimarisha ukusanyaji, uchambuzi na usambazaji wa takwimu za hali ya hewa pamoja na kuboresha mifumo ya utoaji wa tahadhari za mapema.
Mafunzo hayo yanafanyika katika Ukumbi wa Best Western Hotel, kuanzia tarehe 19 hadi 21 Januari 2026.

