Jamhuri ya Muungano wa Tanzania

MAMLAKA YA HALI YA HEWA TANZANIA

ISO 9001:2015 Imethibitishwa Kutoa Huduma za Hali ya Hewa kwenye Usafiri wa Anga

TMA NA BRAC MAENDELEO TANZANIA WAJADILI MIKAKATI YA KUIMARISHA USAMBAZAJI NA MATUMIZI YA TAARIFA ZA HALI YA HEWA

News Image

Dodoma, Mei 15, 2026 
Mamlaka ya Hali ya Hewa Tanzania (TMA)  na BRAC Maendeleo Tanzania walifanya kikao Makao Makuu ya TMA jijini Dodoma, wakijadili mikakati ya kuimarisha usambazaji na matumizi ya taarifa za hali ya hewa nchini. 

Kikao hicho kiliongozwa na Mkurugenzi Mkuu wa Mamlaka ya Hali ya Hewa Tanzania (TMA) na Makamu Mwenyekiti wa Jopo la Kimataifa la Sayansi ya Mabadiliko ya Hali ya Hewa na Tabianchi (IPCC), Dkt. Ladislaus Chang’a, kwa kuwakaribisha wajumbe wa BRAC Maendeleo Tanzania na kueleza kuwa TMA inathamini ushirikiano na wadau katika kuboresha huduma za hali ya hewa. Alisema mkutano huo unatoa fursa ya taasisi hizo mbili kuelewana na kuchunguza maeneo ya ushirikiano katika huduma za hali ya hewa, tahadhari za mapema na hatua za kukabiliana na mabadiliko ya tabianchi. Pia alieleza kuwa TMA ipo katika mageuzi ya kidigitali yanayolenga kuboresha utoaji wa huduma kwa njia za kisasa.

Dkt. Chang’a Alieleza dhamira ya TMA kuendelea kuboresha huduma za hali ya hewa na ushawishi wa Tanzania katika maduala ya hali ya hewa katika bara la Africa na ukanda wa Nchi zinazoendelea.  Aliwashukuru BRAC kwa majadiliano yenye tija na kwa mchango wao katika kuelimisha Jamii na kuimarisha usambazaji wa Taarifa za hali ya hewa kwa jamii. Alisisitiza na kuhamasisha ushiriki wa WADAU wengi katika Mkutano wa nne wa Shirika la Hali ya Hewa Duniani (WMO) Unaolenga kuboresha miongozo ya Utabiri wa Hali ya Hewa (Operational Climate Prediction OCP-4) na Unatarajiwa kufanyika Arusha kuanzia 29 Juni hadi 3 Julai 2026.

Kwa upande wake Bw. Degefu Getachew Kelbiso, Meneja Mwandamizi wa Programu ya Hali ya Hewa ya Kimataifa na BRAC Maendeleo Tanzania, alieleza kuhusu mpango wa “BigBet” unaolenga kukabiliana na mabadiliko ya tabianchi kupitia huduma za taarifa za hali ya hewa, kilimo kinachozingatia mabadiliko ya hali ya hewa na tabianchi, masoko na uimarishaji wa maisha ya jamii katika nchi kadhaa ikiwemo Tanzania. 

Bw. Degefu alieleza haja ya kuimarisha ushirikiano katika kuendelea kuboresha upatikanaji, usambazaji,  tafsiri  na matumizi ya taarifa za hali ya hewa  kwa watumiaji wa mwisho na katika sekta zote za kiuchumi na kijamii  na katika miradi ya jamii na maendeleo.