Jamhuri ya Muungano wa Tanzania

MAMLAKA YA HALI YA HEWA TANZANIA

ISO 9001:2015 Imethibitishwa Kutoa Huduma za Hali ya Hewa kwenye Usafiri wa Anga

TANZANIA YAANDAA MKUTANO WA NNE WA KIMATAIFA WA WATAALAMU WA HALI YA HEWA DUNIANI.

News Image

TANZANIA YAANDAA MKUTANO WA NNE WA KIMATAIFA WA WATAALAMU WA HALI YA HEWA DUNIANI. 
Arusha, Tanzania – Juni 29, 2026

Jamhuri ya Muungano wa Tanzania imeweka historia ya kuwa mwenyeji wa mkutano wa  Nne wa kimataifa wa wataalamu bingwa  wa hali ya hewa Duniani ulioandaliwa na Shirika la Hali ya Hewa Duniani (WMO) kwa kushirikiana na Mamlaka ya Hali ya Hewa Tanzania(TMA), kwa lengo la kuimarisha utabiri wa hali ya hewa, mifumo ya tahadhari za mapema na huduma za hali ya hewa kwa maendeleo endelevu.
Akifungua mkutano huo, mgeni rasmi Waziri wa Uchukuzi, Mhe. Prof. Makame Mnyaa Mbarawa (Mb), alisema Tanzania inajivunia kuwa mwenyeji wa mkutano huu muhimu, akisema hatua hiyo inaonesha kuongezeka kwa mchango wa Afrika katika mijadala ya kimataifa kuhusu mabadiliko ya hali ya hewa na tabianchi na kuimarisha huduma za hali ya hewa.
"Tunajivunia Tanzania kuwa mwenyeji wa mkutano huu muhimu, ikizingatiwa kuwa unafanyika barani Afrika kwa mara ya kwanza. Hii inaonyesha nafasi ya Afrika inayozidi kukua katika mijadala ya kimataifa kuhusu mabadiliko ya hali ya hewa na tabianchi na inaonesha umuhimu wa kuimarisha huduma za hali ya hewa katika bara letu."

Aidha, Mh.Prof. Mbarawa (Mb) aliendelea kuelezea Jitihada na uwekezaji mkubwa wa Serikali  katika kuimarisha miundombinu ya hali ya hewa na mifumo ya uangazi wa hali ya hewa chini ya uongozi ya Mh.Raisi Samia Suluhu,ikiwa ni sehemu ya dhamira yake ya kuboresha huduma za utabiri wa hali ya hewa nchini

Naibu Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Mhe. James Kinyasi Millya, alisisitiza dhamira ya Tanzania ya kuendeleza ushirikiano wa kimataifa katika sayansi ya hali ya hewa, akisema uamuzi wa kuandaa mkutano huo nchini unaonyesha imani ambayo jumuiya ya kimataifa inaendelea kuiweka kwa Tanzania.

Naye Naibu Katibu Mkuu wa Shirika la Hali ya Hewa Duniani (WMO) Dkt. Ko Barrett, alisistiza  kuwa mkutano huo ni fursa na jukwaa muhimu la kujadili maendeleo ya sayansi ya hali ya hewa na namna bora ya kuimarisha ufanisi na tija katika huduma za utabiri wa hali ya hewa. Aidha aliendelea kusisitiza umuhimu na mchango wa matumizi ya teknolojia, ikiwemo matumizi ya Akili Mnemba (AI), katika kuboresha utabiri wa hali ya hewa. 

Awali, Mkurugenzi Mkuu wa Mamlaka ya Hali ya Hewa Tanzania (TMA) na Makamu Mwenyekiti  wa Jopo la Kimataifa la Sayansi ya Mabadiliko ya Hali ya Hewa na Tabianchi (IPCC), Dkt. Ladislaus Chang'a, alisema kuwa mahitaji ya taarifa sahihi na za kuaminika za hali ya hewa yanaendelea kuongezeka  kutokana na changamoto ya mabadiliko ya hali ya hewa na tabianchi na hususan kuongezeka kwa idadi na ukubwa wa matukio ya hali mbaya ya hewa. Taarifa za mapema na za uhakika zinasaidia kufanya maamuzi ya haraka na yenye tija, hususan kwa jamii zilizo katika mazingira hatarishi.

Mkutano huo unatarajiwa kuleta matokea chanya katika kuimarisha ushirikiano wa kimataifa, kuboresha mifumo ya utabiri wa hali ya hewa  na kuimarisha huduma za hali ya hewa katika sekta zote za kiuchumi na kijamii ikiwemo kilimo, rasilimali za maji, nishati, uchukuzi na usimamizi wa athari za maafa, sambamba na kuunga mkono utekelezaji wa mpango wa Umoja wa Mataifa wa Tahadhari za Mapema kwa Wote (Early Warnings for All).