Habari

Imewekwa: Oct, 17 2025

UTABIRI WA MVUA ZA MSIMU NOVEMBA 2025 HADI APRILI 2026 WATOLEWA RASMI

UTABIRI WA MVUA ZA MSIMU NOVEMBA 2025 HADI APRILI 2026 WATOLEWA RASMI

Dar es Salaam, Tarehe 17 Oktoba, 2025

Mamlaka ya Hali ya Hewa Tanzania (TMA) imetoa rasmi utabiri wa mvua za msimu kwa maeneo yanayopata mvua mara moja kwa mwaka. Maeneo hayo ni mikoa ya Kigoma, Katavi, Singida, Dodoma, Rukwa, Songwe, Mbeya, Iringa, Njombe, Lindi, Mtwara, Ruvuma na Kusini mwa Morogoro katika kipindi cha miezi ya Novemba, 2025 hadi Aprili, 2026.

Akitoa utabiri huo kwa vyombo mbalimbali vya habari katika ukumbi wa Ubungo Plaza, Kaimu Mkurugenzi Mkuu, TMA na Makamu Mwenyekiti wa Jopo la Kimataifa la Sayansi ya Mabadiliko ya Hali ya Hewa na Tabianchi (IPCC), Dkt. Ladislaus Chang’a alisema Mvua za Chini ya Wastani hadi Wastani zinatarajiwa katika mikoa ya Kigoma, Tabora, Katavi, Singida na Dodoma. Aidha, mvua za Wastani hadi Chini ya Wastani zinatarajiwa katika mikoa ya Njombe, Iringa, Mbeya, Songwe, Rukwa, Ruvuma, Mtwara na Lindi pamoja na kusini mwa mkoa wa Morogoro.

“Mvua zinatarajiwa kuanza kati ya wiki ya tatu na ya nne ya mwezi Oktoba, 2025 katika mikoa ya Tabora, Katavi na Kigoma; na kusambaa katika mikoa ya Rukwa, Songwe, Mbeya, Iringa, Njombe pamoja na kusini mwa mkoa wa Morogoro kati ya wiki ya pili na ya tatu ya mwezi Novemba, 2025 na zinatarajiwa kuisha kati ya wiki ya nne ya mwezi Aprili na wiki ya kwanza ya mwezi Mei 2026 katika maeneo mengi” Alifafanua Dkt. Chang’a.

“Msimu unatarajiwa kutawaliwa na vipindi virefu vya ukavu na mtawanyiko wa mvua usioridhisha katika maeneo mengi japo Kipindi cha nusu ya pili ya msimu (Februari – Aprili, 2026) kinatarajiwa kuwa na ongezeko la mvua ikilinganishwa na nusu ya kwanza (Novemba, 2025 – Januari, 2026)”. Aliongezea Dkt. Chang’a.

Akieleza athari zinazoweza kujitokeza, Dkt. Chang’a alisema Mvua za Chini ya Wastani zinazotarajiwa katika maeneo mengi zinaweza zikasababisha upungufu wa unyevu wa udongo, jambo ambalo linaweza kuathiri ukuaji na maendeleo ya mazao na kupunguza mavuno hususani kwa mazao yanayotegemea mvua. Aidha, kupungua kwa kina cha maji kwenye mabwawa na mtiririko wa maji kwenye mito kunaweza kutokea, hali ambayo inaweza kupunguza upatikanaji wa maji kwa matumizi mbalimbali huku upatikanaji wa maji na malisho kwa ajili ya mifugo ukitarajiwa kuathirika.

Kwa maelezo kamili kuhusu utabiri huu tembelea: https://www.meteo.go.tz/uploads/publications/sw1760695853-Mwelekeo%20wa%20mvua%20za%20Msimu%20(Novemba,%202025-Aprili,%202026).pdf