Habari

Imewekwa: Nov, 28 2025

HALI YA JOTO KALI NCHINI

HALI YA JOTO KALI NCHINI

Dar es Salaam, 28 Novemba, 2025:

Mamlaka ya Hali ya Hewa Tanzania (TMA) inapenda kutoa taarifa ya hali la joto katika maeneo mbalimbali nchini.

Kumekuwepo na ongezeko la Joto katika baadhi ya maeneo hapa nchini hususan yale yanayopata misimu miwili ya mvua kwa mwaka kwa miezi ya hivi karibuni. Hali hii imesababishwa na kusogea kwa Jua la Utosi sambamba na upungufu wa mvua unaojitokeza katika maeneo hayo. Kwa kawaida vipindi vya Jua la Utosi nchini hufikia kilele mwishoni mwa mwezi Novemba wakati Jua la Utosi likiwa linaelekea kusini (Tropiki ya Kaprikoni) na hali hiyo hujirudia tena mwezi Februari wakati Jua la Utosi likiwa linaelekea kaskazini (Tropiki ya Kansa). Jua la Utosi huambatana na hali ya ongezeko la Joto kwa sababu uso wa Dunia katika eneo tajwa huwa karibu zaidi na Jua kuliko maeneo mengine.

Katika kipindi cha mwezi Novemba, 2025 hali ya ongezeko la Joto imeendelea kujitokeza katika baadhi ya maeneo nchini, ambapo hadi kufikia tarehe 27 Novemba, 2025 kituo cha hali ya hewa cha Moshi (Kilimanjaro) kiliripoti kiwango cha juu zaidi cha nyuzi joto 35.7°C mnamo tarehe 21 Novemba, 2025 ikiwa ni ongezeko la nyuzi joto 4.2°C ukilinganisha na wastani wa muda mrefu kwa mwezi Novemba katika kituo hicho. Kituo cha hali ya hewa cha Ilonga (Morogoro) kiliripoti nyuzi joto 35.5°C mnamo tarehe 20 Novemba (ongezeko la nyuzi joto 2.7°C). Kituo cha hali ya hewa Morogoro kiliripoti nyuzi joto 34.5°C mnamo tarehe 26 Novemba (ongezeko la nyuzi joto 2.3°C). Kituo cha Ibadakuli (Shinyanga) kiliripoti nyuzi joto 33.6°C mnamo tarehe 14 Novemba (ongezeko la nyuzi joto 2.2°C), na Dar es salaam nyuzi joto 33.2 °C mnamo tarehe 19 na 21 Novemba (ongezeko la nyuzi joto 1.6°C).

Aidha, ongezeko la unyevu angani (Relative humidity) katika kipindi hiki linalosababishwa na mvuke wa Bahari hususan katika maeneo ya ukanda wa pwani na maeneo jirani limechangia pia mwili kuhisi joto zaidi ya viwango vinavyoripotiwa.

Hata hivyo, katika kipindi cha mwezi Desemba, 2025 vipindi vya mvua vinatarajiwa kujitokeza katika maeneo mengi nchini. Hali hii inatarajiwa kusababisha kupungua kwa Joto katika baadhi ya maeneo hususan yanayopata misimu miwili ya mvua kwa mwaka.

Kwa taarifa hii wananchi wanashauriwa kuendelea kuzingatia taarifa na tahadhari za hali mbaya ya hewa zinazotolewa na Mamlaka ya Hali ya Hewa Tanzania sambamba na kutafuta, kupata na kufuata ushauri wa wataalam katika sekta husika ili kupunguza athari zinazotokana na hali mbaya ya hewa.