Seasional Forecast
UTABIRI WA MVUA ZA MSIMU (NOVEMBA, 2026 – APRILI, 2027)
Dondoo muhimu za mvua za Msimu (Novemba, 2026 – Aprili, 2027)
Taarifa hii inatoa uchambuzi wa mwenendo wa mifumo ya hali ya hewa na mwelekeo wa mvua za Msimu kwa maeneo yanayopata msimu mmoja wa mvua kwa mwaka (kanda ya magharibi, kati, nyanda za juu kusini magharibi, kusini mwa nchi, ukanda wa pwani ya kusini pamoja na maeneo yaliyopo kusini mwa Mkoa wa Morogoro) katika kipindi cha miezi ya Novemba, 2026 hadi Aprili, 2027. Ushauri na tahadhari umetolewa kwa wadau wa sekta mbalimbali wanaotumia taarifa za hali ya hewa katika utekelezaji wa majukumu yao kama vile kilimo na usalama wa chakula, mifugo na uvuvi, maliasili, wanyamapori na utalii, nishati na maji, ujenzi, usafiri na usafirishaji (nchi kavu, kwenye maji na angani), mamlaka za miji, afya, sekta binafsi pamoja na menejimenti za maafa. Muhtasari wa mwelekeo wa mvua hizo na athari zake ni kama ifuatavyo:
a) Mwelekeo wa mvua za Msimu kwa maeneo yanayopata msimu mmoja wa mvua kwa mwaka:
- Mvua za Msimu 2026/2027 zinatarajiwa kuathiriwa kwa kiwango kikubwa na hali ya El Niño yenye Nguvu Kubwa, hususan nusu ya kwanza ya msimu (Novemba 2026 hadi Januari 2027).
- Mvua za Juu ya Wastani hadi Wastani zinatarajiwa katika mikoa ya Kigoma, Tabora, Katavi, Singida, Dodoma, Njombe, Iringa, Mbeya, Songwe, Rukwa pamoja na maeneo ya kusini mwa mkoa wa Morogoro. Hata hivyo, mvua za Wastani hadi Juu ya Wastani zinatarajiwa katika mikoa ya Ruvuma, Mtwara na Lindi.
- Mvua za Msimu zinatarajiwa kuanza wiki ya nne ya mwezi Oktoba katika baadhi ya maeneo ya mikoa ya Tabora, Katavi, Kigoma, Lindi na Mtwara na kusambaa katika maeneo mengine mwezi Novemba 2026. Mvua hizi zinatarajiwa kuisha kati ya wiki ya tatu na ya nne ya mwezi Aprili, 2027 katika maeneo mengi.
- Mvua nyingi zinatarajiwa katika kipindi cha nusu ya kwanza ya msimu (Novemba, 2026 – Januari, 2027), ikilinganishwa na nusu ya pili (Februari – Aprili, 2027).
b) Athari na ushauri
- Vipindi vya unyevu kwenye udongo wa kuzidi kiasi pamoja na mafuriko vinaweza kujitokeza na kuathiri ukuaji wa mazao na miundombinu ya kilimo.
- Ongezeko la kina cha maji katika mabwawa na mito linatarajiwa kujitokeza, hali ambayo inaweza kuathiri miundombinu ya rasilimali za maji na nishati.
- Magonjwa ya mlipuko yanaweza kujitokeza kutokana na uchafuzi wa maji.
Kwa taarifa zaidi tafadhali pakua

