Habari
VULI 2024: MVUA ZINATARAJIWA KUANZA KWA KUSUASUA NA KUTAWALIWA NA VIPINDI VIREFU VYA UKAVU.
Dar es Salaam, 22/08/2024;
Mamlaka ya Hali ya Hewa Tanzania (TMA) imetoa utabiri wa msimu wa mvua za VULI 2024 kwa maeneo yanayopata mvua mara mbili kwa mwaka. Akizungumza wakati wa mkutano na vyombo mbalimbali vya habari, Kaimu Mkurugenzi Mkuu wa TMA na Makamu Mwenyekiti wa Jopo la Kimataifa la Sayansi ya Mabadiliko ya Hali ya Hewa na Tabianchi Dkt. Ladislaus Chan’ga alisema maeneo yanayopata mvua mara mbili kwa mwaka ni Mikoa ya Arusha, Manyara na Kilimanjaro, Mikoa ya Dar es Salaam, Pwani, maeneo ya kaskazini mwa mkoa wa Morogoro pamoja na visiwa vya Unguja na Pemba, Mikoa ya Kagera, Geita, Mwanza, Shinyanga, Simiyu na Mara pamoja na kaskazini mwa mkoa wa Kigoma.
Dkt Chang’a alisema mvua za Vuli kwa mwaka huu 2024 zinatarajiwa kuanza kwa kusuasua zikitawaliwa na vipindi virefu vya ukavu, aliongezea kuwa maeneo mengi yanatarajiwa kupata mvua za chini ya wastani hadi wastani huku vipindi vya joto kali kuliko kawaida vikitarajiwa.
“Mvua za Vuli kwa mwaka huu 2024 zinatarajiwa kuanza kwa kusuasua,zikitawaliwa na vipindi virefu vya ukavu na mtawanyiko wake ukitarajiwa kuwa usioridhisha katika maeneo mengi, ingawa maeneo mengi yanatarajiwa kupata mvua za chini ya wastani hadi wastani japo izingatiwe kuwa matukio ya vipindi vifupi vya mvua kubwa yanaweza kujitokeza katika maeneo machache na vipindi vya joto kali kuliko la kawaida vinaweza kujitokeza”. Alisisitiza Dkt. Chang’a
Akizungumza kuhusu athari zinazotarajiwa kujitokeza, Dkt. Chang’a alisema upungufu wa unyevunyevu kwenye udongo unatarajiwa kujitokeza katika maeneo mengi, wadudu na magonjwa ya mazao yanatarajiwa kuongezeka, aliwashauri wakulima kutumia mbinu na teknolojia za kilimo himilivu za kuhifadhi maji na unyevunyevu wa udongo sambamba na kupata ushauri kwa maafisa ugani. Kwa upande wa mifugo alisema upungufu wa mvua unatarajiwa kuathiri upatikanaji wa maji na malisho kwa ajili ya mifugo, hali inayoweza kupelekea kujitokeza kwa migogoro baina ya wafugaji na watumiaji wengine wa ardhi kutokana na upungufu wa maji na malisho hivyo alishauri jamii kuweka mpango mzuri wa matumizi na uhifadhi wa maji pamoja na malisho.
Utabiri wa msimu wa mvua za vuli 2024 unapatikana katika ofisi zote za TMA nchini pamoja na mitandao ya mawasiliano kama vile TMA online TV, tovuti, blog, facebook na Instagram.
Kwa taarifa zaidi tembelea; https://www.meteo.go.tz/uploads/publications/sw1724321444-Mwelekeo%20wa%20Mvua%20za%20Vuli%202024.pdf