Habari

Imewekwa: Sep, 02 2022

VULI 2022: MVUA ZA CHINI YA WASTANI HADI WASTANI ZINATARAJIWA KATIKA MAENEO MENGI YA NCHI.

VULI 2022: MVUA ZA CHINI YA WASTANI HADI WASTANI ZINATARAJIWA KATIKA MAENEO MENGI YA NCHI.

Dar es Salaam; Tarehe 2 Septemba, 2022;

Mamlaka ya Hali ya Hewa Tanzania (TMA) imetoa rasmi utabiri wa msimu wa mvua za Vuli 2022 kwa maeneo yanayopata mvua mara mbili kwa mwaka. Akizungumza wakati wa mkutano na vyombo vya habari katika Makao Makuu ya TMA, Ubungo Plaza, Tarehe 2/9/2022, Mkurugenzi Mkuu wa TMA na Makamu wa tatu wa Rais wa Shirika la Hali ya Hewa Duniani (WMO), Dkt. Agnes Kijazi alisema maeneo ya nchi yanayopata misimu miwili ya mvua yanatarajiwa kupata mvua za chini ya wastani hadi wastani.

“Kutokana na mifumo ya hali ya hewa ilivyo kwa sasa na inavyotarajiwa katika kipindi chote cha msimu, kwa ujumla mvua za chini ya wastani hadi wastani zinatarajiwa katika maeneo mengi ya nchi yanayopata misimu miwili ya mvua kwa mwaka. Msimu unatarajiwa kuanza kwa kuchelewa na kuambatana na mtawanyiko wa mvua usioridhisha. Vipindi virefu zaidi vya ukavu vinatarajiwa katika miezi ya Oktoba na Novemba 2022, hata hivyo vipindi vya ongezeko kidogo la mvua vinatarajiwa kujitokeza katika maeneo machache hususan wiki ya tatu na ya nne mwezi Disemba, 2022. Kwa kawaida msimu wa mvua za Vuli huisha mwezi Disemba. Hata hivyo, kunatarajiwa kuwepo na muendelezo wa mvua kwa mwezi Januari, 2023”. Alieleza Dkt Kijazi

Vilevile Dkt. Kijazi alisema kuwa matarajio ya Vipindi vya joto kali kuliko kawaida katika msimu wa Vuli vinatarajiwa.“Pamoja na matarajio yamvua za chini ya wastani hadi wastani, ongezeko la joto linatarajiwa katika msimu wa Vuli hususani katika Maeneo ya kaskazini mwa mkoa wa Morogoro, mikoa ya Pwani (ikijumuisha visiwa vya Mafia), Dar es Salaam, Tanga pamoja na visiwa vya Unguja na Pemba) na Mikoa ya Arusha, Manyara na Kilimanjaro” Alisema Dkt Kijazi.

Taarifa hiyo pia imetoa angalizo la mvua kubwa kwa baadhi ya maeneo nchini. “Ingawa maeneo mengi yanatarajiwa kupata mvua za chini ya wastani hadi wastani, izingatiwe kuwa matukio ya vipindi vifupi vya mvua kubwa yanaweza yakajitokeza katika maeneo machache, watumiaji wa taarifa za utabiri huu wanashauriwa pia kufuatilia utabiri wa saa 24, siku 10 pamoja na mwezi kama unavyotolewa na Mamlaka ya hali ya Hewa Tanzania.” Alizungumza Dkt Kijazi

Akimaliza kutoa taarifa hiyo, Dkt. Kijazi alisema, Mamlaka ya Hali ya Hewa Tanzania itaendelea kufuatilia mwenendo wa mifumo ya hali ya hewa na kutoa mirejesho ya mwelekeo wa mvua nchini kadri inavyohitajika. Aidha, wadau wanashauriwa kuwasiliana na Mamlaka ili kupata taarifa mahsusi za utabiri wa msimu ili kukidhi mahitaji maalum katika sekta zao.