Jamhuri ya Muungano wa Tanzania

MAMLAKA YA HALI YA HEWA TANZANIA

ISO 9001:2015 Imethibitishwa Kutoa Huduma za Hali ya Hewa kwenye Usafiri wa Anga

TMA YAWAPA MWANGA TANESCO KUKABILIANA NA EL NIÑO

News Image

TMA YAWAPA MWANGA TANESCO KUKABILIANA NA EL NIÑO

4 Septemba 2026 ,Dodoma.


Shirika la Umeme Tanzania (TANESCO) limefanya ziara katika ofisi ya Makao Makuu ya Mamlaka ya Hali ya Hewa Tanzania (TMA), kwa lengo la kujengewa uwezo na kupata uelewa wa kitaalamu kuhusu hali ya hewa ya El Niño, athari zake na namna bora ya kutumia taarifa za hali ya hewa katika kuchukua hatua za mapema za kukabiliana na athari zinazoweza kujitokeza.


Ziara hiyo iliwaleta pamoja wataalamu kutoka TANESCO, ambapo Mkurugenzi Mkuu wa TMA, ambaye na Makamu Mwenyekiti wa Jopo la Kimataifa la Sayansi ya Mabadiliko ya Hali ya Hewa na Tabianchi (IPCC), Dkt. Ladislaus Chang’a, alitoa  ufafanuzi wa kina kuhusu hali ya El Niño, mwenendo wa hali ya hewa na athari zinazoweza kuambatana na matukio ya hali mbaya ya hewa.


Dkt. Chang’a alisisitiza umuhimu wa Shirika la Umeme Tanzania kuendelea kutumia taarifa za hali ya hewa katika mipango yake, hususan katika kuimarisha miundombinu ya umeme ili kupunguza athari za mvua kubwa.

“Ni muhimu kuimarisha miundombinu ya umeme, hususan nguzo, ili kupunguza athari za mvua kubwa na upepo mkali unaoweza kusababisha kuanguka kwa nguzo na kukatika kwa huduma ya umeme.”Alisema Dkt.Chang'a

Katika majadiliano hayo, wataalamu kutoka TANESCO waliuliza maswali kuhusu El Niño, maeneo yanayoweza kuathirika, mwenendo wa mvua na namna taarifa za TMA zinavyoweza kutumika katika kupanga na kuchukua hatua za mapema za kupunguza athari.


Kwa upande wake Mkuu wa Msafara kutoka TANESCO, Bw. Anthony Mbushi, aliipongeza TMA kwa kutoa elimu kuhusu El Niño na hali ya hewa, akisema elimu hiyo itasaidia TANESCO katika kupanga na kutekeleza shughuli zake kwa ufanisi .

“Tunawashukuru kwa kutupatia fursa hii ya kujifunza na kuongeza uelewa wetu kuhusu masuala ya El Niño na hali ya hewa kwa ujumla. Ushauri na elimu tuliyoipata tutaufanyia kazi katika shughuli na miradi yetu. Pia tunawapongeza kwa kuendelea kuhakikisha umma na wadau mbalimbali wanapata taarifa za hali ya hewa kwa wakati”. Alisema Bw. Anthony


Mamlaka ya Hali ya Hewa Tanzania (TMA) inaendelea kuweka kipaumbele katika kuwaelimisha na kuwajengea uwezo wadau mbalimbali kuhusu El Niño na matukio mengine ya hali mbaya ya hewa, ili kuwawezesha kuchukua hatua za mapema na sahihi za kujikinga na kupunguza athari zinazoweza kujitokeza.