Habari

Imewekwa: Oct, 05 2021

TMA YAKUTANA NA WADAU WA MADINI KUJENGA UELEWA WA UTEKELEZAJI WA KANUNI ZA SHERIA NA.2 YA 2019 YA TMA

TMA YAKUTANA NA WADAU WA MADINI KUJENGA UELEWA WA UTEKELEZAJI WA KANUNI ZA SHERIA NA.2 YA 2019  YA TMA

Dodoma; Tarehe 29 – 30 Septemba, 2021;

TMA imekutana na wadau wa sekta ya madini nchini ili kujenga uelewa wa pamoja wa utekelezaji wa Kanuni za Sheria ya Mamlaka ya Hali ya Hewa Tanzania Na.2 ya 2019. Mkutano huo ulifanyika katika ukumbi wa PSSSF (Makale), Dodoma, Tarehe 29 - 30 Septemba 2021.

Akizungumza wakati akifungua mkutano wa Wadau wa Madini mgeni rasmi, ambaye ni mwakilishi wa Katibu Mkuu Wizara ya Ujenzi na Uchukuzi (Sekta ya Uchukuzi) Bw. Himidu Mbegu alisema kanuni hizo zimekamilika na zipo tayari kwa utekelezaji.

“Wizara kwa kushirikiana na Mamlaka ya Hali ya Hewa Tanzania imekamilisha kanuni saba za sheria Na.2 ya 2019. Utekelezaji wa kanuni hizi katika sekta ya madini utasaidia kupunguza madhara yanayotokana na matukio ya hali ya hewa migodini kupitia matumizi ya taarifa mahsusi na sahihi za hali ya hewa”. Alizungumza Bw. Mbegu.

Aidha, Bw. Mbegu alisema TMA imeandaa mifumo ya kufungasha na kufikisha huduma kwa wadau wa sekta ya madini sambamba na mfumo wa kusajili vituo vya hali ya hewa nchini kwa kuzingatia masharti ya kanuni juu ya uwekaji na uendeshaji wa vituo vya hali ya hewa ili kupata takwimu sahihi kwa matumizi mapana ya sekta ya hali ya hewa na wadau wake.

Awali, wakati akimkaribisha mgeni rasmi, Dkt. Agnes Kijazi, Mkurugenzi Mkuu wa TMA na Makamu wa Tatu wa Rais wa Shirika la Hali ya Hewa Duniani (WMO) alieleza jukumu la Mamlaka ya Hali ya Hewa na umuhimu wa kikao hicho cha wadau wa madini.

“Mamlaka ya Hali ya Hewa Tanzania ina jukumu la kuhakikisha inatoa huduma za hali ya hewa zilizo bora kwa wadau mbalimbali ikiwepo sekta ya madini. Hivyo, kikao hiki ni muhimu kwasababu kitagusa maeneo mawili muhimu ya kisheria na tayari yapo katika kanuni, ambayo ni umiliki wa vituo vya hali ya hewa na uchangiaji wa huduma za hali ya hewa zinazotolewa na Mamlaka ya Hali ya Hewa katika sekta ya madini nchini”. Alisema Dkt. Kijazi.

Kwa upande wa wadau, waliishukuru TMA kwa ushirikishwaji wa mkutano huu wa kujenga uelewa wa pamoja wa utekelezaji wa kanuni za Sheria ya Mamlaka ya Hali ya Hewa Tanzania Na.2 ya 2019 na kusema matumizi ya taarifa za hali ya hewa katika sekta ya madini ni muhimu hivyo Mamlaka itoe elimu zaidi ili kupata uelewa wa pamoja kwa wadau wote.

Naye, Mkurugenzi wa Huduma za Sheria Wizara ya Ujenzi na Uchukuzi Adv. Mohamed Salum akizungumza wakati wa kufunga mkutano huo, aliwashukuru wadau wa sekta ya madini kwa kushiriki mkutano huo wa kujenga uelewa wa utekelezaji wa kanuni za TMA zilizokuwa chini ya Sheria ya Mamlaka ya Hali ya Hewa Tanzania Na.2 ya 2019 na kukiri kuwa wadau wameonesha uelewa mkubwa na umuhimu juu ya utekelezaji wa sheria hii na namna itakavyowasaidia katika utekelezaji wa majukumu yao ya kila siku ya uchimbaji wa madini na kuonesha kwamba uhitaji wa taarifa za hali ya hewa ni jambo la muhimu kabla ya kuanza shughuli zao.