Habari
TMA YAHIMIZWA KUONGEZA JITIHADA ZA KUIFIKISHIA JAMII TAARIFA ZA HALI YA HEWA KWA WAKATI
Mbeya; Tarehe 05 Agosti, 2022;
Mamlaka ya Hali ya Hewa Tanzania (TMA), imehimizwa kuongeza jitihada za kuifikishia jamiitaarifa za hali ya hewa kwa wakati, hayo yalizungumzwa na Mkuu wa Wilaya ya Songea, Mhe. Pololet Kamando Mgema akimuwakilisha Mkuu wa Mkoa wa Ruvuma Mhe. Kanali Laban Elias Thomas alipotembelea banda la TMA, tarehe 5 Agosti 2022 kupitia maonesho ya Nane Nane yanayoendelea kufanyika katika viwanja vya John Mwakangale, Uyole - Mbeya kuanzia tarehe 1 hadi 8 Agosti, 2022.
“Kazi yenu inajitangaza kwa kuwa mmekuwa mnafanya vizuri katika utabiri wenu wa msimu hivyo nawapongeza sana, lakini niwahimize kuongeza jitihada za kuwafikishia jamii taarifa hizo za hali ya hewa kwa wakati ziweze kutumika na kuwasaidia kwa wakati. Alisisitiza Mhe. Pololet Mgema.
Naye Mkuu wa Wilaya ya Mbinga Mhe. Aziza Mangosongo akiongozana na Mhe. Pololet Mgema aliongezea kwa kuipongeza TMA kwa utabiri mzuri wanaoutoa na kufanya wananchi kuwa na imani na taarifa za hali ya hewa kwa kuzitumia katika shughuli zao za kiuchumi na kijamii.
Aidha, akielezea namna TMA ilivyoboresha utabiri wa hali ya hewa katika ngazi ya wilaya kupitia vyombo vya habari, Ndg. Isack Yonah, Meneja wa Huduma za Hali ya Hewa Kilimo alisema, Sheria ya Mamlaka ya Hali ya Hewa Tanzania, Namba 2 ya mwaka 2019 imeipa Mamlaka jukumu la kutoa huduma, kudhibiti na kuratibu shughuli za hali ya hewa katika Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, na tayari imeshaboresha vifaa na mitambo ya hali ya hewa inayotumia teknolojia ya kisasa inayosaidia upatikanaji wa taarifa za hali ya hewa zilizo sahihi zinazokusanywa katika vituo vya hali ya hewa ikiwemo kituo cha hali ya hewa kinachojiendesha chenyewe (Automatic Weather Station-AWS) ambacho kimeletwa kwenye maonesho hayo.
Ndg. Isack Yonah aliongezea kuwa katika uboreshaji wa huduma za hali ya hewa, TMA inatoa utabiri wa hali ya hewa hadi ngazi ya wilaya na hata kama ikitokea mkulima au mdau yeyote atahitaji kujua hali ya hewa ya eneo lake anaweza kuandaliwa taarifa mahususi kulingana na mahitaji yake kwa kuchangia huduma hiyo ili kufanya huduma hizo ziendelee kuwa endelevu.