Habari

Imewekwa: Oct, 22 2021

TMA WAJIPANGA KUTOA UTABIRI KATIKA NGAZI YA WILAYA

TMA WAJIPANGA KUTOA UTABIRI KATIKA NGAZI YA WILAYA

Dar es Salaam, Tarehe 21/10/2021

“Utabiri huu wa Msimu utaambatana na utabiri katika ngazi ya Wilaya zilizomo kwenye maeneo yanayopata msimu mmoja wa mvua. Hivyo, nawapongeza sana TMA kwa hatua hii kubwa ya kuongeza wigo wa utoaji utabiri hususani kwa watumiaji wa taarifa za hali ya hewa wa sekta mbalimbali ambao wamekuwa na uhitaji wa taarifa za utabiri wa maeneo madogo madogo kwenye maeneo yao kwa kutumia fursa mbali mbali zilizopo”. Dkt. Buruhani Nyenzi, Mwenyekiti wa Bodi ya Mamlaka ya Hali ya Hewa Tanzania (TMA) aliyasema hayo wakati akifungua mkutano wa wadau wa Utabiri wa Mvua za Msimu wa Vuli(Novemba, 2021 hadi Aprili, 2022) wenye kauli mbiu ya “Matumizi sahihi ya utabiri wa maeneo madogomadogo kwa ukuaji wa uchumi wa viwanda”, katika Ukumbi wa Chuo cha Taifa cha Usafirishaji (NIT).

Aidha, ili taarifa hizi za utabiri zilizoandaliwa kwa kila wilaya, ziwe na tija iliyokusudiwatunahitajikuipatia Mamlaka ushirikiano katika kuhakikisha kwamba taarifa hizi zinawafikia watumiaji wa mwisho kwenye sekta mbalimbali ili kuweza kuchangia katika ukuaji wa uchumi. Pia alisema wanapojiandaa kupokea taarifa ya Utabiri wa Msimu wa Mvua wa Novemba 2021 hadi April, 2022 ni muhimu sana kila mmoja kufuatilia kwa karibu, kuelewa, kupanga na kukabiliana na hali ya hewa inayotarajiwa katika sekta yake. Aliongezea Dkt. Nyenzi

Kwa upande wake Dkt. Agnes Kijazi, Mkurugenzi Mkuu Mamlaka ya Hali ya Hewa Tanzania na Makamu wa Tatu wa Rais wa Shirika la Hali ya Hewa Duniani (WMO) amesema kuwa ni vyema kila wilaya na kila sekta ikatumia taarifa za hali ya hewa katika kufanya maamuzi sahihi na kuweka mipango ili kuboresha huduma zao kwa lengo la kuongeza tija na pia kupunguza athari za hali mbaya ya hewa inapojitokeza.

Aidha, wadau wameipongeza Mamlaka kwa jitihada za kuhakikisha kuwa taarifa hizi za hali ya hewa zinawafikia walengwa wakuu na pia wameitaka Mamlaka kuongeza wigo wa kuifikia jamii ili ipate taarifa kwa wakati na pale inapotokea mabadiliko ya utabiri wa hali ya hewa.