Jamhuri ya Muungano wa Tanzania

MAMLAKA YA HALI YA HEWA TANZANIA

ISO 9001:2015 Imethibitishwa Kutoa Huduma za Hali ya Hewa kwenye Usafiri wa Anga

UJUMBE WA MKURUGENZI MKUU WA TMA DKT. LADISLAUS CHANG’A KATIKA SIKU YA HALI YA HEWA DUNIANI, TAREHE 23 MACHI, 2026.

News Image

Leo tunaungana na jumuiya ya kimataifa kuadhimisha Siku ya Hali ya Hewa Duniani (World Meteorological Day – WMD). Mamlaka ya Hali ya Hewa Tanzania (TMA), ikiwa Mamlaka ya Kitaifa yenye jukumu la kutoa huduma za hali ya hewa kwa umma, taasisi mbalimbali na watumiaji binafsi wa huduma maalum kwa ajili ya maendeleo ya kijamii na kiuchumi, pamoja na kusimamia na kuratibu shughuli za hali ya hewa katika mipaka ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania na kutoa tahadhari na ushauri kuhusu matukio ya hali mbaya ya hewa kwa lengo la kulinda maisha ya watu na mali zao, inaungana na jumuiya ya hali ya hewa duniani kote kuadhimisha Siku ya Hali ya Hewa Duniani kwa mwaka 2026. Maadhimisho ya mwaka huu ni kumbukizi ya miaka 76 tangu kuanzishwa kwa Shirika la Hali ya Hewa Duniani (WMO) tarehe 23 Machi 1950. Tanzania ni mojawapo ya nchi wanachama 193 wa WMO, ambapo kupitia TMA inaendelea kuthibitisha dhamira yake thabiti ya kuimarisha huduma za hali ya hewa ambazo ni msingi muhimu wa usalama, ustawi wa jamii na maendeleo endelevu ya taifa.

Kaulimbiu ya Siku ya Hali ya Hewa Duniani mwaka huu ni: “Pima hali ya hewa leo, ili kesho iwe salama" (Observing Today, Protecting Tomorrow)”. Kaulimbiu hii inalenga kusisitiza umuhimu wa kuimarisha mifumo ya uangazi wa hali ya hewa na matumizi sahihi ya data za hali ya hewa zinazokusanywa ili kuwezesha maamuzi yenye tija katika sekta mbalimbali za kijamii na kiuchumi. Taarifa hizi zimeendelea kusaidia kuongeza uzalishaji, usalama na ustahimilivu wa jamii yetu kwa sasa na kwa vizazi vijavyo. Kaulimbiu hii pia inatukumbusha sisi wataalamu wa hali ya hewa, wataalamu wa rasilimali maji, wanasayansi, watunga sera na wadau mbalimbali kuwa, uangazi na ufuatiliaji wa mifumo ya hali ya hewa ni msingi wa kazi zote tunazozifanya. Kuanzia vituo vya uangazi wa ardhini na anga za juu, RADA na mitandao ya uangazi wa maji, mifumo hii hutuwezesha kuelewa mienendo ya mifumo ya hali ya hewa, kutambua hatari zinazoweza kujitokeza, na kutoa taarifa sahihi za hali ya hewa pamoja na tahadhari za mapema kwa wakati muafaka. Kwa kufanya hivyo, tunachangia kwa kiasi kikubwa kuokoa maisha ya watu na mali zao, pamoja na kusaidia maendeleo endelevu ya kijamii na kiuchumi ya taifa letu.

Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, imeendelea kufanya uwekezaji mkubwa wa kimkakati katika huduma za hali ya hewa ambao ni muhimu kwa kuimarisha ustahimilivu wa taifa dhidi ya athari za mabadiliko ya hali ya hewa ikiwa ni pamoja na tahadhari dhidi ya matukio ya hali mbaya ya hewa yanayoendelea kuongezeka kwa ukubwa na idadi kutokana na mabadiliko haya. Serikali imeendelea kuboresha miundombinu ya hali ya hewa katika mnyororo mzima wa utoaji wa huduma hizi nchini. Miongoni mwa uwekezaji huo ni pamoja na ujenzi unaoendelea wa Jengo la Kanda ya Mashariki ambalo litatumika pia kama Kituo cha Tahadhari za Tsunami; pia ujenzi wa Kituo cha Uhakiki wa Vifaa vya Hali ya Hewa (Instrument Calibration Centre) jijini Dar es Salaam. Aidha, Serikali imeendelea kuboresha na kuongeza vifaa vya kisasa vya uangazi wa hali ya hewa ili kuimarisha usahihi wa data za hali ya hewa, ufuatiliaji mifumo na utabiri wa hali ya hewa.

Miongoni mwa mafanikio yaliyopatikana katika uwekezaji katika sekta ya hali ya hewa nchini ni pamoja na uwekaji wa Rada tano (5) za hali ya hewa zilizoko Mwanza, Dar es Salaam, Mtwara, Kigoma na Mbeya kati ya Rada saba (7) zilizopangwa katika mtandao wa kitaifa wa Rada za hali ya hewa. Aidha, Serikali imenunua na kufunga vifaa mbalimbali vya kisasa vya hali ya hewa ikiwa ni pamoja na: Vifaa 10 vya hali ya hewa kwa ajili ya usafiri wa anga (Aviation Meteorological Systems (AVIMET); Vituo 50 vya hali ya hewa vinavyojiendesha vyenyewe (Automatic Weather Stations – AWS); Vipima mvua 60 vinavyojiendesha vyenyewe (Automatic rain gauges); Vituo 15 vya kisasa vya hali ya hewa kwa ajili ya huduma za hali ya hewa-kilimo (Agrometeorological AWS).

Serikali pia imewezesha ufungaji wa Kompyuta yenye uwezo mkubwa wa kuchakata taarifa (High Performance Computer – HPC) ambayo imeimarisha sana uchakataji na uchambuzi wa data za hali ya hewa na kuboresha shughuli za utabiri na uandaaji wa taarifa mahsusi za hali ya hewa kwa watumiaji na sekta mbalimbali. Vilevile, mfumo wa kisasa wa utabiri wa hali ya hewa (forecasting system) umefungwa ili kuimarisha uchakataji wa data na taarifa na kuongeza usahihi wa utabiri wa hali ya hewa hivyo kusaidia kulinda maisha ya watu na kuendeleza shughuli mbalimbali za kiuchumi.

Vilevile, TMA pia imeendelea kushikilia cheti cha ubora cha ISO 9001:2015 katika utoaji wa huduma za hali ya hewa kwa usafiri wa anga, na hivyo kuendelelea kuthibitisha ubora wa huduma mahususi za hali ya hewa kwa ajili usafiri wa anga.

Kwa upande wa ushiriki na mchango wetu kimataifa, TMA imeendelea kuiwakilisha Tanzania ipasavyo katika majukwaa mbalimbali ya kimataifa ambapo wataalamu 15 wa Tanzania wanahudumu katika vikosi kazi na kamati mbalimbali za Shirika la Hali ya Hewa Duniani (WMO) pamoja na Jopo la Kimataifa la Sayansi ya Mabadiliko ya Hali ya Hewa (IPCC).

Kwa mfano: Dkt. Ladislaus Chang’a, Mkurugenzi Mkuu wa TMA, alichaguliwa mwezi Julai 2023 kuwa Makamu Mwenyekiti wa IPCC kwa kipindi cha miaka saba; Dkt. Pascal Waniha, Mkurugenzi wa Miundombinu na Huduma za Ufundi wa TMA, anahudumu kama Makamu Rais wa Kamisheni ya WMO ya uangazi , miundombinu na ubadilishajaji wa data na taarifa za hali ya hewa (WMO Commission on Observation, Infrastructure, and Information Systems-INFCOM) tangu mwaka 2024; Dkt. Hamza Kabelwa, Mkurugenzi wa Huduma za Utabiri, anahudumu kama Mwenyekiti Mwenza wa Kamati ya WMO inayoshughulikia mfumo jumuishi wa WMO wa uchakataji wa taarifa za hali ya hewa na utabiri (WMO Standing Committee on WMO Integrated Processing and Prediction System (SC-WIPPS)) tangu mwaka 2024. Ushiriki wa wataalamu hawa katika ngazi na vyombo hivi muhimu vya kimataifa ni kudhihirisha mchango mkubwa wa Tanzania katika kuandaa na kutekeleza kanuni na miongozo ya utoaji wa huduma za hali ya hewa duniani.

Katika juhudi za kuimarisha huduma za hali ya hewa nchini, TMA haijabaki nyumba katika matumizi ya teknolojia za kisasa ikiwemo matumizi ya Akili Mnemba (Artificial Intelligence – AI) ili kuboresha utoaji wa huduma na mifumo ya utoaji wa maamuzi katika sekta mbalimbali nyeti hususan zile zinazoathiriwa sana na hali ya hewa na kwa umma kwa ujumla. Katika kukabiliana na mabadiliko na maendeleo ya kiteknolojia, wataalamu wa TMA wamebuni mifumo ambayo ni pamoja na; Mfumo wa mawasiliano na ubadilishanaji wa taarifa na data za hali ya hewa kutoka vituo vya hali ya hewa kote nchini na kuzikusanya kwenye kituo kikuu cha utabiri kilichopo Dar es Salaam kabla ya kubadilishana nan chi nyingine duniani ujulikanao kwa jina “Digital Meteorological Observatory (DMO)”, pia mfumo wa ukusanyaji na usambazaji wa taarifa za hali ya hewa kwa watumiaji wa bahari na maziwa “Marine Meteorological Information System (MMIS)” na mfumo wa mawasiliano ya taarifa za hali ya hewa kwa sekta ya usafiri wa anga “Meteorological Aviation Information System (MAIS)” . Ubunifu huu umeimarisha uangazi, usimamizi wa data za hali ya hewa, usambazaji wa taarifa hizi na utoaji wa huduma. Juhudi hizi ni utekelezaji wa kazi zetu sambamba na dira ya TMA ya kuwa  “Kitovu bora cha huduma za hali ya hewa kwa maendeleo endelevu ya kiuchumi na kijamii”

Katika Nyanja za Kikanda na Kimataifa, Mamlaka ya Hali ya Hewa ya Tanzania inaendelea kutoa usaidizi wa kiufundi kwa Taasisi nyingine za Hali ya Hewa za nchi nyingine hususan za barani Afrika katika maeneo muhimu ya sekta hii ya hali ya hewa, ikiwa ni pamoja na uboreshaji wa Mfumo wa Usimamizi wa Ubora (Quality Management System-QMS) na Tathmini ya Wataalamu (Competence-based Assessment) na mafunzo kuhusu mifumo ya TMA ya DMO, na MAIS. Kwa siku za karibuni, TMA imetoa usaidizi wa kiufundi kwa baadhi ya Taasisi za Hali ya Hewa za Afrika Mashariki na Kusini mwa Afrika kwa kushirikiana na Shirika la Hali ya Hewa Duniani (WMO) kupitia programu zake za kikanda barani Afrika.Nchi tulizosaidia ni pamoja na; Burundi na Sudani Kusini,Namibia na Zimbabwe. Matarajio yetu ni TMA kuwa kitovu bora barani Afrika cha kukuza ujuzi na uvumbuzi katika sekta ya hali ya hewa.

Kwa kutambua pia umuhimu wa elimu kwa wataalamu wa hali ya hewa katika kuboresha huduma za tahadhari za hali ya hewa, TMA inasimamia na kuendesha Chuo cha Taifa cha Hali ya Hewa “National Meteorological Training Centre (NMTC)” kilichopo Mkoani Kigoma. Chuo cha NMTC kina ithibati ya NACTE na kina jukumu la kutoa mafunzo kwa wataalamu ikiwa ni pamoja na mafunzo ya uangazi na ufuatiliaji wa mifumo ya hali ya hewa, matumizi ya taarifa za Rada za hali ya hewa, Teknolojia ya Habari na Mawasiliano (TEHAMA) na mabadiliko ya hali ya hewa na tabianchi kwa ngazi za cheti na stashahada. Mafunzo ya ngazi za juu, kuanzia ngazi ya Shahada ya kwanza hadi Shahada ya Uzamivu, yanapatikana kupitia ushirikiano wa TMA na taasisi za elimu ya juu za kitaifa na kimataifa ikiwa ni pamoja na Chuo Kikuu cha Dar es Salaam (UDSM) na Chuo Kikuu cha Sayansi na Teknolojia cha Nelson Mandela (NM-AIST) kilichopo Jijini Arusha.

Ili kuimarisha zaidi mitandao ya uangazi wa hali ya hewa, Tanzania inaendelea kuimarisha ushirikiano na washirika mbalimbali wa maendeleo na mashirika ya kimataifa, ikiwa ni pamoja na Shirika la Hali ya Hewa Duniani (WMO). Kupitia TMA, Tanzania inaendelea na utekelezaji wa Programu ya WMO ya “Systematic Observing Financing Facility (SOFF)” yenye lengo la kuwekeza katika miundombinu ya uangazi wa hali ya hewa kwa nchi zinazoendelea. Uwekezaji huu utaimarisha ufuatiliaji na uangazi wa hali ya hewa na kuboresha uwezo wa kutoa tahadhari za mapema na hivyo kuimarisha ustahimilivu wa jamii zilizo hatarini dhidi ya mabadiliko ya hali ya hewa na tabianchi.

Tunapoadhimisha Siku ya Hali ya Hewa Duniani 2026, napenda kusisitiza tena kuhusu dhamira thabiti ya TMA ya kuendelea kuimarisha mifumo ya uangazi wa hali ya hewa kwa kipindi tulichonacho ili tuweze kulinda maisha ya watu na mali zao kwa maendeleo endelevu ya kijamii na kiuchumi kwa kesho yetu.

Nachukua fursa hii kutoa shukrani zangu za dhati kwa Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kwa uwekezaji mkubwa wa kuendelea kuimarisha huduma za hali ya hewa hapa nchini. Pia tunaendelea kuwashukuru Wadau mbalimbali wa Maendeleo, wa Kitaifa na Kimataifa, Vyombo vya Habari pamoja na Wafanyakazi wote wa TMA kwa juhudi zao kubwa na mchango wao katika kuendeleza huduma za hali ya hewa kitaifa, kikanda na kimataifa.

Tuendelee kushirikiana kuimarisha uangazi wa hali ya hewa leo kwa usalama wa kesho yetu. Siku ya Hali ya Hewa Duniani inatukumbusha kuwa, masuala ya hali ya hewa na maji yanatuunganisha binadamu wote. Na kuwa kila utabiri wa hali ya hewa tunaotoa, kila tahadhari inayotolewa, na kila data na taarifa ya hali ya hewa tunazokusanya na kubadilishana; vyote vina lengo moja kuu: kulinda ustawi wa maisha yetu ya sasa na baadaye.

“Pima hali ya hewa leo, ili kesho iwe salama" (Observing Today, Protecting Tomorrow)”