Habari

Imewekwa: Jun, 05 2024

SERIKALI YAFURAHISHWA NA UFANISI WA KAZI WA TMA

SERIKALI YAFURAHISHWA NA UFANISI WA KAZI WA TMA

  1. Dodoma; Tarehe 5 Juni, 2024;

Makamu wa Rais wa Tanzania Mh. Dkt. Philip Isdor Mpango ameipongeza Mamlaka ya Hali ya Hewa Tanzania (TMA) kwa ufanisi mkubwa wa kazi ya kutoa huduma za hali ya hewa, zinazosaidia sekta za kiuchumi na kijamii nchini . Aliyasema hayo alipotembelea banda la TMA kwenye Kilele cha Maadhimisho ya Wiki ya Mazingira Duniani, yanayo fanyika katika viwanja vya JICC, Dodoma.

Dkt. Mpango ambaye alikuwa mgeni rasmi katika kilele cha Maadhimisho haya muhimu, Alitembelea banda la TMA na aliambatana na Waziri Mkuu wa Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Kassim Majaliwa, na Waziri wa Mazingira Ofisi ya Makamu wa Rais Mhe. Selemani Jafo.“Hongereni sana Mamlaka ya Hali ya Hewa Tanzania, na kama nilivyosema mwanzo, tunaona utofauti mkubwa sana, ufanisi wenu wa kazi umeongezeka, tunaona matunda ya uwekezaji ambao serikali imefanya kwani taarifa zenu zina uhakika” Alisema Dkt Mpango.

Kwa upande wake Kaimu Mkurugenzi Mkuu wa TMA na Makamu mwenyekiti wa jopo la kimataifa la sayansi ya mabadiliko ya hali ya hewa na tabia nchi, Dkt Ladislaus Chang’a aliishukuru Serikali ya awamu ya sita inayoongozwa na Rais Dkt Samia Suluhu Hassan kwa mwendelezo wa uwekazaji unaoendelea kufanya kwenye sekta ya hali ya hewa nchini.“Napenda kuishukuru Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kwa uwekezaji wa mkubwa unaoendelea kufanywa kwenye sekta yetu ya hali ya hewa nchini. Ndani ya miaka mitatu Tanzania imefanya uwekezaji mkubwa wa maendeleo kwenye sekta ya hali ya hewa kupita nchi zote za Afrika Mashariki na Kati. Mpaka mwanzoni mwa mwaka ujao tutakuwa na Rada saba za hali ya hewa” Alisema Dkt Chang’a

Aidha, Dkt Chang’a alimaliza kwa kumhakikishia Makamu wa Rais na Watanzania wote kwa ujumla kwamba, Mamlaka ya Hali ya Hewa itaendelea kuongeza ufanisi katika ufuatiliaji wa mifumo ya hali ya hewa nchini na kutoa taarifa za uhakika na kwa wakati. “Ujumbe wetu kwa watanzania Mheshimiwa Makamu wa Rais ni kuwasisitizia watanzania wote kuendelea kufuatilia na kuzingatia taarifa bora na rasmi za hali ya hewa zinazotolewa na TMA pamoja na kuzingatia maagizo na maelekezo yanayotolewa na viongozi wa Serikali kipindi cha matukio ya hali mbaya ya hewa.” Alisema Dkt.Chang’a

Mamlaka inaendelea kuwakaribisha wananchi na wadau wote kutoka sekta mbalimbali nchini kwenye Maadhimisho ya Wiki ya Mazingira Duniani.Huduma zote za hali ya hewa zinaendela kutolewa kwenye banda la TMA.