Habari

Imewekwa: Oct, 29 2022

MWENYEKITI WA BODI TMA APONGEZA UTEKELEZAJI WA MKATABA WA BARAZA LA WAFANYAKAZI.

MWENYEKITI WA BODI TMA APONGEZA UTEKELEZAJI WA MKATABA WA BARAZA LA WAFANYAKAZI.

Kibaha, Pwani; Tarehe 29 Oktoba, 2022;

Mwenyekiti wa Bodi ya Mamlaka ya Hali ya Hewa Tanzania (TMA), Dkt. Buruhani Nyenzi ameipongeza TMA kwa kutekeleza Mkataba wa Baraza kwa kuhakikisha wajumbe wa Baraza wanakutana mara mbili kwa mwaka. Alieleza hayo wakati akifungua rasmi Baraza la Wafanyakazi wa TMA la pili kwa mwaka 2022 katika Ukumbi wa Manesi na Wakunga,Kibaha, Pwani, tarehe 29/10/2022.

“Kupitia taarifa ya Mwenyekiti wa Baraza, nimeelezwa kuwa hiki ni kikao cha pili, hivyo naipongeza Mamlaka kwa kuwa na mabaraza mawili kwa mwaka kulingana na Mkataba. Aidha, niendelee kuwapongeza kwa uwakilishi mzuri kwa kuwa na wajumbe tisini na nane kutoka maeneo mbalimbali nchini”. Alisema Dkt. Nyenzi.

Dkt. Nyenzi aliendelea kwa kuipongeza Mamlaka kwa utekelezaji mzuri wa miradi mikubwa na mafanikio yaliyopatikana hususani fanikio la kuboresha miundo mbinu ya hali ya hewa sambamba na kutekeleza agizo la Serikali la kuhamia Dodoma, Makao Makuu ya nchi. Vilevile, aliishukuru Bodi kwa kazi nzuri ya usimamizi wa Taasisi uliochangia mafanikio hayo.

“Nitumie fursa hii kuwashuruku wajumbe wa Bodi ambao nimefanya nao kazi kwa kipindi cha miaka mitatu kwa utumishi wao uliotukuka uliopelekea mafanikio yote haya yaliyoainishwa na Mwenyekiti wa Baraza hili, ikiwa ni pamoja na uboreshaji wa maslahi ya wafanyakazi”. Alieleza Dkt. Nyenzi.

Awali, Mkurugenzi wa Utafiti na Matumizi Dkt. Ladislaus Chang’a, akisoma taarifa ya Mwenyekiti wa Baraza kwa niaba ya Dkt. Agnes Kijazi, Mkurugenzi Mkuu wa TMA na Makamu wa tatu wa Rais wa Shirika la Hali ya Hewa Duniani (WMO), alishukuru Serikali kupitia Wizara na Bodi ya TMA kwa ushirikiano na kazi kubwa iliyofanyika ya kufanikisha malengo ya Taasisi, ambapo viwango vya usahihi wa utabiri vimeendelea kuongezeka, nakutoa wito kwa watanzania kutumia taarifa hizo za hali ya hewa.

Katika taarifa hiyo, Dkt. Kijazi aliendelea kueleza kuwa “Dhumuni kuu la Baraza hili ni kufanya tathmini ya utendaji wa Mamlaka ambao utasaidia kuongeza ubora na ufanisi katika utoaji wa huduma kwa umma kwa lengo la kupunguza athari za mabadiliko ya hali ya hewa na tabia nchi”.

Akielezea baadhi ya mafanikio yaliyopatikana katika kipindi cha Baraza lililopita na Baraza la sasa, Mwenyekiti wa Baraza alisema mafanikio hayo ni pamoja na “ufanisi wa utekelezaji wa sheria ya Mamlaka ya Hali ya Hewa na Kanuni zake, ununuzi wa rada na miundo mbinu kwa ujumla, uboreshaji wa maslahi ya wafanyaki kwa kuendelea kupandishwa vyeo,kubadilishwa kada,ongezeko la mishahara na kuhuishwa kwa miundo ya kada kwa watumishi kufuatia mabadiliko ya Miundo ya Maendeleo ya Watumishi”.