Jamhuri ya Muungano wa Tanzania

MAMLAKA YA HALI YA HEWA TANZANIA

ISO 9001:2015 Imethibitishwa Kutoa Huduma za Hali ya Hewa kwenye Usafiri wa Anga

MHE. KAKOSO ATOA WITO KWA WATANZANIA KUFUATILIA NA KUZINGATIA TAARIFA ZA HALI YA HEWA.

News Image

Mwenyekiti wa Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Miundombinu Mhe. Selemani Kakoso (MB) ametoa wito kwa watanzania kufuatilia na kuzingatia taarifa za hali ya hewa kutoka Mamlaka ya Hali ya Hewa Tanzania (TMA), kwa kuwa ni muhimu katika kupanga na kutekeleza mipango na shughuli katika sekta zote  za kiuchumi na kijamii hapa nchini, aliyasema hayo wakati wa ziara ya Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Miundombinu katika ofisi ya TMA, Dar es Salaam.

“Natoa wito kwa Watanzania kufuatilia na kuzingatia  taarifa za utabiri zinazotolewa na TMA kabla ya kuanza kutekeleza majukumu yenu katika sekta zenu ikiwemo kilimo, maji au kibiashara kwa kuwa TMA imekuwa ikitoa taarifa za uhakika kila siku kupitia vyombo mbalimbali vya habari. Kutokana na ubora na ufanisi wa huduma zao,  na weledi na umahiri wa wataalamu wake, TMA  wameaminiwa kutoa misaada ya kitaalamu kwa  baadhi ya Taasisi za hali ya hewa katika nchi mbalimbali barani Afrika.” Alisisitiza Mhe. Kakoso

Kupitia ziara hiyo yenye lengo la kukagua miradi inayotekelezwa na TMA, kamati ilipata fursa ya kupokea taarifa ya utekelezaji wa mradi wa ujenzi wa Ofisi ya TMA Kanda ya Mashariki na Kituo cha Tahadhari ya Matukio ya Tsunami pamoja na Kituo cha Taifa cha Uhakiki wa vifaa vya hali ya hewa na baadaye Mamlaka ilielekezwa kuongeza jitihada za usimamizi katika kuhakikisha miradi hiyo inakamilika kwa wakati na kwa ubora unaotakiwa kwa kuzingatia matakwa ya mkataba.

Naye Waziri wa Uchukuzi mwenye dhamana ya kusimamia sekta ya hali ya hewa Prof. Makame Mbarawa (MB) alisema Serikali ya awamu ya sita itaendelea kuwekeza kwenye sekta ya hali ya hewa na kuisimamia kwa karibu. Mh. Mbarawa aliahidi kufuatiilia kwa karibu kuhakikisha kuwa fedha zinazohitajika kwa ajili yya ukamilishaji wa miradi hiyo muhimu ya ujenzi wa miundombinu ya huduma za  hali ya hewa zinapatikana kwa wakati.

Kwa upande wake Mkurugenzi Mkuu, TMA na Makamu Mwenyekiti wa Jopo la Kimataifa la Sayansi ya Mabadiliko ya Hali ya Hewa na Tabianchi, Dkt. Ladislaus Chang’a aliishukuru Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Miundombinu kwa kuwa sababu mafanikio ya TMA yamechagizwa pia na mchango mkubwa wa kamati kutaka kuona changamoto za TMA zinatatuliwa, kupitia maelekezo mbalimbali waliyokuwa wanatoa kwa nyakati tofauti.

“Kupitia ziara ya mwaka 2022 Mwanza, kamati hii iliiongezea nguvu TMA katika kuhakikisha tunaimarisha miundombinu ya hali ya hewa ikiwemo ukamilishaji wa rada 5 za hali ya hewa, mitambo mbalimbali ya kiutendaji, ongezeko la rasilimali watu pamoja na kujengewa uwezo wa kiutendaji wataalam wa hali ya hewa” Alisema Dkt. Chang’a

Dkt. Chang’a aliishukuru Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kwa kuiwezesha Mamlaka katika utekelezaji wa miradi miwili ya ujenzi wa jengo la Ofisi ya TMA Kanda ya Mashariki na Kituo cha Tahadhari ya Matukio ya Tsunami, ambapo ujenzi wake umefikia asilimia 65 pamoja na ujenzi wa Kituo cha Taifa cha Uhakiki wa vifaa vya hali ya hewa ambapo ujenzi wake umefikia asilimia 40. Kukamilika kwa miradi hii miwili kutaifanya TMA kuwa katika nafasi nzuri ya kuwa kitovu cha kuhakiki vifaa vya hali ya hewa hadi Ukanda wa Afrika.