Habari
MATOKEO YA AWALI YA KILICHOKUWA KIMBUNGA HAFIFU “JOBO”
.jpeg)
Dar es Salaam, 25 Aprili 2021 Alasiri
Taarifa hii inaelezea matokeo ya kilichokuwa kimbunga hafifu “Jobo” katika mifumo ya hali ya hewa na maeneo mbalimbali hapa nchini.
Kimbunga hafifu “Jobo” kilitarajiwa kuingia nchi kavu katika maeneo ya mikoa ya ukanda wa Pwani leo tarehe 25/04/2021. Alfajiri ya leo tarehe 25/04/2021 kimbunga hafifu “Jobo” kilifika karibu na eneo la pwani ya mikoa ya Dar es Salaam na Pwani kikiwa kimepoteza nguvu yake baada ya kukutana na ongezeko la upepo kinzani. Hivyo, kiwango kikubwa cha mvua ilivyotarajiwa kuambatana na kimbunga “Jobo” imeonekana kunyesha zaidi baharini ambapo viwango vya mvua vinafika milimita 250 katika muda wa saa 24 na kupunguza athari za moja kwa moja za mvua hiyo katika eneo la nchi kavu. Aidha, vipindi vifupi vya upepo mkali vilijitokeza ambapo upepo ulioripotiwa baharini ulifikia kasi ya kilometa 40 hadi 50 kwa saa katika pwani ya Kilwa na Mtwara kabla ya kimbunga “Jobo” kupungua nguvu.
Kwa upande mwingine, kimbunga hicho kiliweza kutawala na kuathiri mwenendo wa mifumo ya hali ya hewa hapa nchini. Hali hiyo, ilisababisha baadhi ya maeneo hata yaliyo mbali na pwani kupata ongezeko la mvua ambapo viwango vikubwa kiasi vya mvua katika kipindi cha saa 24 zilizopita hadi kufika saa 3 asubuhi ya leo tarehe 25/04/2021 vimepimwa katika mikoa ya kanda ya Ziwa Victoria. Viwango hivyo vya mvua ni milimita 59 (Musoma) na Milimita 56(Mwanza).
Kwa sasa, mabaki ya mawingu yaliyoambatana na kilichokuwa kimbunga “Jobo” bado yapo baharini na yanaendelea kusababisha vipindi vya mvua katika maeneo machache ya ukanda wa pwani. Hali ya mvua inatarajiwa kuendelea katika muda uliosalia wa siku ya leo tarehe 25/4/2021 na kesho Jumatatu tarehe 26/4/2021. Aidha, mvua za msimu zinatarajiwa kuendelea katika maeneo yanayopata mvua hizo.