Habari

Imewekwa: May, 08 2023

ELIMU YA HALI YA HEWA YATOLEWA KWA WATU WENYE UHITAJI MAALUM

ELIMU YA HALI YA HEWA YATOLEWA KWA WATU WENYE UHITAJI MAALUM

Mamlaka ya Hali ya Hewa Tanzania kwa kushirikiana na Shirikisho la Vyama vya Walemavu Tanzania (SHIVYAWATA) imewajengea uwezo watu wenye uhitaji maalumu kwa kutoka elimu ya masuala mbalimbali ya Hali ya Hewa ikiwemo uchambuzi wa hali ya hewa kuanzia ngazi ya uangazi hadi usambazaji, Elimu hii pia ilihusisha aina mbalimbali za utabiri wa hali ya hewa kuanzia utabiri wa muda mfupi, kati, mwezi, msimu, hali mbaya ya hewa na athari zake, mabadiliko ya hali ya hewa na tabia nchi pamoja na majukumu ya Mamlaka, kupitia warsha iliyofanyika katika Ukumbi wa Chuo cha Maendeleo ya Wananchi (FDC), Ikwiriri, Rufiji.

Akizungumza wakati wa mafunzo hayo, Katibu wa SHIVYAWATA Rufiji Bwana Abdul Warusimbi aliishukuru TMA kwa kufika Ikwiriri na kuweza kutoa elimu ambayo itawasaidia katika kukabiliana na majanga yatokanayo na hali mbaya ya hewa kwa washiriki 100 kutoka Rufiji, Nyamisati na Visiwa vya Chole na Mafia.

“Katika siku za hivi karibuni kumetokea majanga mbalimbali ambayo yamesababishwa na mabadiliko ya hali mbaya ya hewa, majanga hayo yamekuwa yakiwaathiri watu wenye ulemavu kwa kiasi kikubwa hususani watu wa vijijini.Kupitia TMA wamejifunza kuwa kila hatua ya maisha wanayopiga wanahitaji usaidizi wa utabiri wa hali ya hewa”Alisema Abdul Warusimbi.

Kwa upande wake, Bwana. Haji Omari Mpili maarufu kama Mzee Mpili, alisema TMA ina wataalamu waliobobea katika masuala ya hali ya hewa na kuwataka wananchi wa Kusini kuacha kutumia utabiri wa kizamani wa kusoma nyota na kujikita katika utabiri wa kisayansi ambao unafanyiwa utafiti wa kitaalamu.

“Mfano hivi sasa msimu wa mvua unaisha lakini kuna watu wengine wanaendelea kupanda. Je, mimea hiyo itafanikiwa? taarifa za hali ya hewa kutoka TMA zinaeleza mvua itaanza kipindi gani na itamalizika kipindi gani, ni vizuri kufuatilia taarifa hizo zenye uhakika”. Alisema Mzee Mpili.

Akizungumza mara baada ya mafunzo hayo, Bwana. Hassan Said Bakari, Mkuu wa Kituo cha Hali ya Hewa Kilwa Masoko, alisema utabiri wa msimu wa mvua ulitabiriwa kuwa chini ya wastani kwa maeneo ya Kusini mwa nchi na kuwataka wananchi kufuatilia taarifa za hali ya hewa kupitia vyombo mbalimbali vya habari.

“Mamlaka imepokea maoni mbalimbali yaliyotolewa na watu wenye uhitaji maalumu na kupitia maoni yao, TMA itayafanyia kazi ili kuhakikisha kundi hili maalum linafikiwa kwa urahisi, vilevile Mamlaka imeendelea kuwakumbuhsha kufuatilia taarifa za hali ya hewa zionazotolewa mara kwa mara ili kuweza kufanya uzalishaji wenye tija hususan kipindi hiki cha changamoto za mabadiliko ya hali ya hewa na tabia nchi”.Alisema Bw. Bakari

Bi. Lulu Salimu, mkazi na mkulima kutoka Ikwiriri alieleza namna ambavyo alitumia taarifa za hali ya hewa zilizitolewa mwezi Oktoba 2023 na kufanya maamuzi ya kutumia mbegu za muda mfupi, hivyo kufanikiwa kupata mavuno mengi wakati wakulima wengine wakipata hasara kutokana na kutumia mbegu za muda mrefu.