Habari

Imewekwa: Feb, 17 2021

DKT. KIJAZI AONGOZA MKUTANO WA KUJADILI VIPAUMBELE KATIKA MPANGO MKAKATI WA WMO WA KUJENGA UWEZO.

DKT. KIJAZI AONGOZA MKUTANO WA KUJADILI VIPAUMBELE KATIKA MPANGO MKAKATI WA WMO WA KUJENGA UWEZO.

Dar es Salaam; Tarehe 03/02/2021.

Mkurugenzi Mkuu wa Mamlaka ya Hali ya Hewa Tanzania (TMA) na Makamu wa Tatu wa Rais wa Shirika la Hali ya Hewa Duniani (WMO), Dkt. Agnes Kijazi, ameongoza mkutano wa pili wa Jopo la Kamati Kuu ya WMO ya Kujenga Uwezo “Second Meeting of the WMO Executive Council Capacity Development Panel (CDP-2)”.

Akizungumza wakati akifungua rasmi mkutano huo, Dkt. Kijazi aliwataka wajumbe wa mkutano huo, kuzingatia lengo lililokasimiwa kwa jopo la kushauri namna bora ya kujenga uwezo katika uboreshaji wa huduma za hali ya hewa Duniani.

“Mkutano huu umelenga kujadili taarifa za utekelezaji wa majukumu ya Vikosi kazi vinavyounda Jopo hili, na kuandaa mapendekezo ya kuwasilisha kwenye Kamati Kuu ya WMO (WMO Executive Coincil (EC), na mapendekezo ya maeneo ya vipaumbele kwa ajili ya kuandaa Mpango Mkakati wa kujenga uwezo (WMO Capacity Development Strategy) katika utoaji huduma Kimataifa”. Alizungumza Dkt. Kijazi.

Katika hatua nyingine, Dkt. Kijazi alimpongeza Katibu Mkuu wa WMO, Prof. Petteri Taalas, kwa kupewa tuzo na jarida la “Reader’s Digest Magazine” kama Mtu Mashuhuri wa Bara la Ulaya wa mwaka 2020 (European of the Year), ikiwa ni kutambua mchango wake wa kuongoza jitihada za WMO kukabiliana na mabadiliko ya hali ya hewa na tabianchi.

Naye, Prof. Taalas alimshukuru Dkt. Kijazi na kusema kuwa tuzo hiyo ni maalum kwa wadau wote wa WMO na huduma za hali ya hewa kwa ujumla na alimpongeza Dkt. Kijazi kwa uongozi wake mahiri unaosaidia kufanikisha utekelezaji wa malengo ya WMO.

Mkutano huo ulifanyika kwa njia ya mtandao (teleconference) Tarehe 3 na 4 Februari, 2021 chini ya Mwenyekiti wa Jopo hilo, Dkt. Kijazi na kuhudhuriwa na Katibu Mkuu wa WMO, Prof. Petteri Taalas na watendaji wengine waandamizi wa WMO. Mkutano ulijadili taarifa za Vikosi kazi vinavyounda jopo hilo na kuandaa mapendekezo mbalimbali ya kujenga uwezo katika huduma za hali ya hewa. Miongoni mwa mapendekezo hayo ni pamoja na yatakayowasilishwa katika mkutano wa 73 wa Kamati Kuu ya WMO namapendekezo ya maeneo ya vipaumbele vitakavyotumika kuandaa Mpango Mkakati wa WMO wa kujenga uwezo. Mjadala ulijielekeza kutambua kwamba hali ya hewa haina mipaka hivyo katika kipindi hiki cha kuongezeka majanga yanayosababishwa na hali mbaya ya hewa jopo hilo lihakikishe vipaombele katika kujenga uwezo vinaelekezwa kuzisadia nchi zinazoendelea pamoja na za Bara la Afrika ili kuhakikisha maendeleo katika sekta ya hali ya hewa hayamuachi mtu yoyote nyuma (no one should be left behind).