Habari

Imewekwa: Jul, 02 2025

DKT CHANG’A AFANYA MAZUNGUMZO YA KITALAMU NA KATIBU MKUU WA SHIRIKA LA HALI YA HEWA DUNIANI (WMO)

DKT CHANG’A AFANYA MAZUNGUMZO YA KITALAMU NA KATIBU MKUU WA SHIRIKA LA HALI YA HEWA DUNIANI (WMO)


Geneva, 2 Julai 2025

Katibu Mkuu wa Shirika la Hali ya Hewa Duniani (World Meteorological Organization - WMO) Prof. Celeste Saulo ameahidi kushirikiana na Mamlaka ya Hali ya Hewa Tanzania (TMA) katika kuboresha huduma za hali ya hewa kwa matumizi katika sekta mbalimbali za kiuchumi na kijamii.

Ameyasema hayo wakati wa kikao baina yake na Dkt. Ladislaus Chang’a, Kaimu Mkurugenzi Mkuu wa Mamlaka ya hali ya Hewa Tanzania (TMA), ambaye pia ni Mwakilishi wa kudumu wa Tanzania katika WMO na Makamu wa Mwenyekiti wa Jopo la Kimataifa la Sayansi ya Mabadiliko ya Hali ya Hewa na Tabianchi (IPCC) wakati wa kikao cha 69 cha Kamati Kuu Tendaji ya IPCC (Intergovernmental Panel on Climate Change-IPCC (69th IPCC Bureau),tarehe 02 Julai 2025 Jijini Geneva, Uswisi. Kikao hicho kilikuwa na lengo la kujadiliana kuhusu maendeleo ya utoaji wa huduma za hali ya hewa na mipango ya kuendeleza ushirikiano.

Prof. Celeste Saulo ameipongeza TMA kwa uwekezaji mkubwa katika sekta ya hali ya hewa kupitia Serikali hususan katika miundombinu ya kisasa ya hali ya hewa na kwa kuendelea kufanya vizuri katika utoaji wa huduma za hali ya hewa nchini pamoja na kusaidia nchi nyingine katika sekta ya hali ya hewa. Prof. Celeste Saulo ameahidi kuendelea kusaidia katika kuboresha huduma za hali ya hewa na mafunzo kwa wataalamu wa hali ya hewa kupitia programu mbalimbali za WMO ikiwa ni pamoja na eneo la mafunzo ya akili mnemba (Artificial Inteligence-AI). Aidha, Prof. Saulo amesisitiza kuwa, Taasisi za Hali ya hewa za nchi wanachama ndizo zenye jukumu mahsusi la kutoa huduma za hali ya hewa katika nchi Wanachama wa WMO hivyo uwekezaji katika sekta hii utaboresha zaidi huduma hizi kwa jamii.

“ Taasisi za hali ya hewa kama TMA ndizo zenye jukumu mahsusi na chanzo cha kuaminika cha huduma za hali ya hewa kwa mujibu wa miongozo ya WMO na napongeza TMA kwa kuendelea kutumia vyema uwekezaji wa Serikali ya Tanzania kutoa huduma bora za hali ya hewa. Pia napongeza TMA kwa kuwa mstari wa mbele kusimamia vyema programu za WMO na kusaidia nchi nyingine kikanda ili kuboresha zaidi huduma huduma za hali ya hewa katika nchi zao na kikanda” Alisema Prof. Celeste Saulo.

Katika Kikao hicho, Dkt. Ladislaus Chang’a ameeleza dhamira ya TMA ya kuboresha huduma za hali ya hewa na kusimamia vyema programu za WMO zinazotekelezwa nchini na kikanda.

“TMA itaendelea kutoa wataalamu wake mahiri kuchangia katika utekelezaji wa programu mbalimbali za WMO kwa manufaa ya Dunia nzima na tutaendelea kusaidia wenzetu hasa katika kanda ya Afrika kwa uzoefu wa utaalamu tulio nao, kwa msaada wa WMO na uwekezaji mkubwa wa Serikali katika tasnia ya hali ya hewa nchini” Alisema Dkt. Chang’a.

Aidha, Dkt. Chang’a alimjulisha Katibu Mkuu wa WMO kuwa, Taasisi za Hali ya Hewa za Nchi wanachama wa WMO ambazo wataalamu wa TMA wametoa msaada wa kiufundi Barani Afrika hivi karibuni ni pamoja na Lesotho, Namibia, Burundi, Zimbabwe na Sudan Kusini, ambapo nchi hizo waliwezeshwa katika maeneo mbalimbali yakiwemo ya uboreshaji wa “Mfumo wa Usimamizi wa Ubora wa huduma (Quality Management System-QMS and Competency Assessment )”, Utabiri wa Hali Mbaya ya Hewa, Utabiri wa Hali ya Hewa kwa Kutumia Modeli za Kihesabu/Kompyuta (Numerical Weather Prediction-NWP)”, “Mchakato wa kisheria katika sekta ya hali ya hewa na Usambazaji wa Huduma za Hali ya Hewa kwa Umma.