Habari

Imewekwa: Sep, 01 2021

BODI TA TMA YAWATAKA WADAU WA HALI YA HEWA KUTOA USHIRIKIANO MZURI KWA TMA

BODI TA TMA YAWATAKA WADAU WA HALI YA HEWA KUTOA USHIRIKIANO MZURI KWA TMA

Dar es Salaam, Tarehe: 31/08/2021

“Ili taarifa hizi za utabiri zilizoandaliwa kwa kila wilaya, ziwe na tija iliyokusudiwatunahitajikuipatia Mamlaka ushirikiano mzuri katika kuhakikisha taarifa hizi zinawafikia watumiaji wa mwisho kwenye sekta mbalimbali ili kuchangia ukuaji wa uchumi hapa nchini”, Makamu Mwenyekiti wa Bodi ya Mamlaka ya Hali ya Hewa Tanzania (TMA), Dkt. Makame O. Makame alisisitiza hayo wakati akifungua rasmi mkutano wa wadau wa utabiri wa msimu wa mvua za vuli (Oktoba hadi Disemba) 2021 uliofanyika katika ukumbi wa mikutano wa ‘Law School’, Dar es Salaam.

Aidha, Dkt. Makame aliendelea kusisitiza kuwa taarifa za hali ya hewa zinalenga kusaidia nchi kufikia malengo ya Mpango wa Taifa katika kujenga uchumi wa viwanda katika eneo la uzalishaji mazao ya chakula na biashara, nishati na maji. Alisema huduma za hali ya hewa zikitumika ipasavyo zitasaidia upatikanaji wa malighafi na nishati kwa viwanda hapa nchini.

Kwa upande wake Mkurugenzi Mkuu wa Mamlaka ya hali ya hewa Tanzania Dkt. Agnes Kijazi amesema kuwa Mkutano huu ni muhimu sana kwa wataalam wa hali ya hewa katika kujifunza kwa undani na kuongeza uelewa wa matumizi sahihi ya taarifa za hali ya hewa katika sekta mbalimbali na hivyo kuendelea kuboresha taarifa zinazotolewa na Mamlaka.

Aidha Dkt. Kijazi aliwakumbusha wadau kuwa TMA inaendelea kufanya utafiti kujua mwenendo wa mvua za mawe zilizojitokeza hivi karibuni katika baadhi ya maeneo hapa nchini, ambapo utafiti huo utasaidia kuboresha utabiri ili kupunguza au kuepusha athari zitokanazo na mvua hizo za mawe.

Pia wadau walioshiriki katika mkutano huo wameipongeza Mamlaka ya Hali ya Hewa Tanzania (TMA) kwa juhudi kubwa wanazozifanya katika kutoa taarifa zilizo sahihi na kwa wakati ambazo wanazitumia katika utekelezaji wa mipango ya sekta zao.

Sekta ambazo zilipata fursa ya kuchangia jinsi walivyoutumia utabiri wa Masika (Machi hadi Mei, 2021) ni pamoja na; Sekta ya Kilimo ambao walisema mazao ya mizizi yaliendelea vizuri katika msimu husika. Sekta ya Maafa walielezea namna utabiri ulivyoleta ufanisi katika njia za kukabiliana na maafa na hivyo kupunguza maafa, Sekta ya afya ambao walisema utabiri ulitumika kwa manufaa katika sekta hiyo. Kwa upande wa Sekta ya Mifugo walisema, miundo mbinu ya ufugaji iliboreshwa ili kukabiliana na athari ambazo zingeweza kujitokeza na Sekta ya Nishati kwa upande wa tafiti za mafuta walisema miradi ya tafiti hizo inaendelea kutumia taarifa za hali ya hewa.