Machapisho

UTABIRI WA MVUA ZA MSIMU (NOVEMBA, 2020 – APRILI, 2021)

Pakua

Dondoo muhimu za mvua za Msimu (Novemba, 2020 – Aprili, 2021)

Taarifa hii inatoa uchambuzi wa mwenendo wa mifumo ya hali ya hewa na mwelekeo wa mvua za Msimu kwa maeneo yanayopata msimu mmoja wa mvua kwa mwaka (kanda ya magharibi, kati, nyanda za juu kusini magharibi, kusini mwa nchi, ukanda wa pwani ya kusini pamoja na maeneo yaliyoko kusini mwa mkoa wa Morogoro) katika kipindi cha miezi ya Novemba, 2020 hadi Aprili, 2021. Ushauri na tahadhari umetolewa kwa wadau wa sekta mbalimbali wanaotumia taarifa za hali ya hewa katika utekelezaji wa majukumu yao kama vile kilimo na usalama wa chakula, mifugo na uvuvi, maliasili, wanyamapori na utalii, nishati na maji, usafirishaji (nchi kavu, kwenye maji na angani), mamlaka za miji, afya pamoja na menejimenti za maafa. Muhtasari wa mwelekeo wa mvua hizo na athari zake ni kama ifuatavyo:

a) Mwelekeo wa mvua za Msimu kwa maeneo yanayopata msimu mmoja wa mvua kwa mwaka:

  1. Mvua zinatarajiwa kuwa za wastani hadi juu ya wastani katika maeneo mengi ya mikoa ya Dodoma, Singida, Mbeya, Songwe, Ruvuma, Njombe, Iringa, Lindi, Mtwara, kusini mwa mkoa wa Morogoro na mashariki mwa mikoa ya Tabora na Katavi. Aidha, maeneo ya mikoa ya Kigoma, Rukwa pamoja na magharibi mwa mikoa ya Tabora na Katavi yanatarajiwa kupata mvua za wastani hadi chini ya wastani.
  2. Vipindi vya mvua nyingi vinatarajiwa katika miezi ya Januari na Aprili 2021.
  3. Mvua zinatarajiwa kuanza katika wiki ya kwanza na ya pili ya mwezi Novemba, 2020 kwa maeneo ya mkoa wa Tabora na kutawanyika katika mikoa mingine inayopata msimu mmoja wa mvua kwa mwaka katika wiki ya tatu ya mwezi Novemba, 2020.
  4. Mvua zinatarajiwa kuisha katika maeneo mengi ya magharibi, kati, nyanda za juu kusini magharibi na pwani ya kusini katika wiki ya nne ya mwezi Aprili, 2021, hata hivyo, kwa mkoa wa Ruvuma mvua zinatarajiwa kuisha kati ya wiki ya pili na ya tatu ya mwezi Aprili, 2021.

b) Athari na ushauri

  1. Hali ya unyevunyevu ardhini inatarajiwa kuwa ya kuridhisha kwa ajili ya kilimo na malisho katika maeneo mengi.
  2. Matukio ya vipindi vifupi vya mvua kubwa yanaweza kusababisha mafuriko na kupelekea uharibifu wa miundombinu, upotevu wa maisha na mali.
  3. Magonjwa ya mlipuko yanaweza kujitokeza kutokana na kutuama kwa maji machafu na uchafuzi wa maji safi.