Karibu

Habari,

Ninayo furaha kubwa kukukaribisha katika Tovuti hii mahususi na rasmi ya Mamlaka ya Hali ya Hewa Tanzania, nikiamini kwa niaba ya Menejimenti na Wafanyakazi wote wa Mamlaka kuwa utapata taarifa mbalimbali zinazoihusu na kutolewa na Mamlaka ambayo ni taasisi pekee iliyopewa dhamana kwa mujibu wa sheria kutoa taarifa mbalimbali za masuala ya hali ya hewa hapa nchini.

Katika Tovuti hii unaweza kupata kuifahamu Mamlaka ya Hali ya Hewa Tanzania, sheria iliyoiunda, anuani zake Makao Makuu na vituo vyetu katika mikoa yote nchini, wigo, upeo wa Mamlaka, dira, dhamira, misingi mikuu na malengo. Tovuti hii inatoa pia nafasi ya kufahamu shughuli za Mamlaka katika maeneo mbalimbali ya kiuchumi na kijamii.

Tovuti hii ya Mamlaka imefanyiwa marekebisho kadhaa na tunaamini ni makubwa ikilinganishwa na Tovuti iliyokuwa ikitumiaka awali, katika maboresho yaliyofanyika tumehakikisha taarifa za utabiri za saa ishirini na nne, siku tano, siku kumi na utabiri wa msimu, utabiri wa siku kumi na wa mwezi mahususi kwa kilimo zinapatikana katika ukurasa wa mbele na unaweza kuzipakua ukihitaji kufanya hivyo. Aidha Mamlaka imehakikisha kunapokuwa na tahadhari ya hali mbaya ya hewa, taarifa hiyo itokee kwa uwazi zaidi na kukushawishi uisome kwanza na baadae uendelee na kutembelea ukurasa ama taarifa uliyokusudia.

Tovuti hii unayotembelea inakupatia fursa ya kupata utabiri wa siku tano kwa angalau ngazi ya mkoa kwa kuchagua mkoa na utapatiwa taarifa hiyo ikiwa katika siku tano.Mamlaka imehakikisha unaweza kupata taarifa za utabiri wa kila siku kwa kuchagua mkoa kupitia kwenye ramani. Katika maboresho Mengine yaliyofanyika ,Tovuti itakupatia fursa ya kupata utabiri kwa njia ya video, utapata pia picha na matukio mbalimbali kupitia ukurasa wa mbele kabisa.

Tovuti hii imeunganishwa na mifumo kadhaa inayotumika katika shughuli za Mamlaka na Tovuti mashuhuri ili kukurahisishia kupata taarifa nyingine.

Mamlaka itaendelea kuboresha Tovuti hii kila itakapobidi ili kuhakikisha wewe mteja ama mdau wetu unapata taarifa nyingi za hali ya hewa kwa matumizi yako kama utakavyokuwa umekusudia.

Asante sana kwa kutembelea Tovuti yetu.

Dkt. Ladislaus Chang'a

Kaimu Mkurugenzi Mkuu