Machapisho

MWELEKEO WA MVUA ZA MSIMU (NOVEMBA, 2025 – APRILI, 2026)

Pakua

Dondoo muhimu za mvua za Msimu (Novemba, 2025 – Aprili, 2026)
Taarifa hii inatoa uchambuzi wa mwenendo wa mifumo ya hali ya hewa na mwelekeo wa mvua za Msimu kwa maeneo yanayopata msimu mmoja wa mvua kwa mwaka (kanda ya magharibi, kati, nyanda za juu kusini magharibi, kusini mwa nchi, ukanda wa pwani ya kusini pamoja na maeneo yaliyopo kusini mwa Mkoa wa Morogoro) katika kipindi cha miezi ya Novemba, 2025 hadi Aprili, 2026. Ushauri na tahadhari umetolewa kwa wadau wa sekta mbalimbali wanaotumia taarifa za hali ya hewa katika utekelezaji wa majukumu yao kama vile kilimo na usalama wa chakula, mifugo na uvuvi, maliasili, wanyamapori na utalii, nishati na maji, ujenzi, usafiri na usafirishaji (nchi kavu, kwenye maji na angani), mamlaka za miji, afya, sekta binafsi pamoja na menejimenti za maafa. Muhtasari wa mwelekeo wa mvua hizo na athari zake ni kama ifuatavyo:

a) Mwelekeo wa mvua za Msimu kwa maeneo yanayopata msimu mmoja wa mvua kwa mwaka:
(i) Mvua za Chini ya Wastani hadi Wastani zinatarajiwa katika mikoa ya Kigoma, Tabora, Katavi, Singida na Dodoma. Aidha, mvua za Wastani hadi Chini ya Wastani zinatarajiwa katika mikoa ya Njombe, Iringa, Mbeya, Songwe, Rukwa, Ruvuma, Mtwara na Lindi pamoja na kusini mwa mkoa wa Morogoro. Msimu unatarajiwa kutawaliwa na vipindi virefu vya ukavu na mtawanyiko wa mvua usioridhisha katika maeneo mengi.
(ii) Mvua zinatarajiwa kuanza kati ya wiki ya tatu na ya nne ya mwezi Oktoba, 2025 katika mikoa ya Tabora, Katavi na Kigoma; na kusambaa katika mikoa ya Rukwa, Songwe, Mbeya, Iringa, Njombe pamoja na kusini mwa mkoa wa Morogoro kati ya wiki ya pili na ya tatu ya mwezi Novemba, 2025. Mvua hizi zinatarajiwa kuisha kati ya wiki ya nne ya mwezi Aprili na wiki ya kwanza ya mwezi Mei 2026 katika maeneo mengi.
(iii) Kipindi cha nusu ya pili ya msimu (Februari – Aprili, 2026) kinatarajiwa kuwa na ongezeko la mvua ikilinganishwa na nusu ya kwanza (Novemba, 2025 – Januari, 2026).

b) Athari na ushauri
(i) Mvua za Chini ya Wastani zinazotarajiwa katika maeneo mengi zinaweza zikasababisha upungufu wa unyevu wa udongo, jambo ambalo linaweza kuathiri ukuaji na maendeleo ya mazao na kupunguza mavuno hususani kwa mazao yanayategemea mvua.
(ii) Kupungua kwa kina cha maji kwenye mabwawa na mtiririko wa maji kwenye mito kunaweza kutokea, hali ambayo inaweza kupunguza upatikanaji wa maji kwa matumizi mbalimbali.
(iii) Upatikanaji wa maji na malisho kwa ajili ya mifugo unatarajiwa kuathirika.