Machapisho

MWELEKEO WA MVUA ZA MSIMU WA VULI ( OKTOBA – DESEMBA), 2025

Pakua

Dondoo muhimu za msimu wa mvua za Vuli kipindi cha Oktoba – Desemba, 2025


Taarifa hii inatoa uchambuzi wa mwenendo wa mifumo ya hali ya hewa na mwelekeo wa msimu wa mvua za Vuli kipindi cha Oktoba - Disemba 2025, ushauri na tahadhari kwa wadau wa Sekta mbalimbali kama vile Kilimo na Usalama wa chakula, Mifugo na Uvuvi, Utalii na Wanyamapori, Usafiri na Usafirishaji (nchi kavu, kwenye maji na angani), Mamlaka za miji, Sekta binafsi, Vyombo vya habari, Nishati, Maji na Madini, Afya pamoja na Menejimenti za maafa. Utabiri huu ni mahsusi kwa maeneo (Nyanda za juu kaskazini mashariki, Pwani ya kaskazini, Ukanda wa Ziwa Viktoria pamoja na kaskazini mwa mkoa wa Kigoma) yanayopata misimu miwili ya mvua kwa mwaka. Kwa muhtasari, mwelekeo huo na athari zake unaonesha kuwa:

a) Mvua za Vuli, 2025
i. Mvua zinatarajiwa kuwa za Wastani hadi Chini ya Wastani katika maeneo mengi na kutawaliwa na vipindi virefu vya ukavu na mtawanyiko wa mvua usioridhisha hususan katika maeneo ya pwani ya kaskazini na nyanda za juu kaskazini mashariki.
ii. Mvua zinatarajiwa kuanza wiki ya kwanza na ya pili ya mwezi Oktoba, 2025 katika maeneo ya mikoa ya Kagera, Geita, Mwanza, Mara na kaskazini mwa mkoa wa Kigoma; na kusambaa katika maeneo ya pwani ya kaskazini na nyanda za juu kaskazini mashariki wiki ya kwanza na ya pili ya mwezi Novemba 2025. Mvua zinatarajiwa kuisha mwezi Januari, 2026.
iii. Mvua za Vuli zinatarajiwa kuongezeka kidogo mwezi Desemba, 2025.
iv. Vipindi vya joto kali kuliko kawaida vinatarajiwa katika msimu huu wa Vuli.


b) Athari zinazotarajiwa
i. Upungufu wa unyevunyevu katika udongo unatarajiwa kujitokeza katika maeneo mengi na hivyo kuathiri shughuli za kilimo.
ii. Kunatarajiwa kupungua kwa kina cha maji katika mito, mabwawa na hifadhi ya maji ardhini.
iii. Kunatarajiwa kujitokeza kwa magonjwa ya mlipuko, kutokana na upungufu wa maji safi na salama.