Machapisho
MWELEKEO WA MSIMU WA KIPUPWE (JUNI-AGOSTI) 2025
PakuaTaarifa hii inatoa uchambuzi wa mwenendo wa mifumo ya hali ya hewa na mwelekeo wa hali ya joto, upepo na mvua katika msimu wa Juni hadi Agosti (JJA), 2025; Ushauri na tahadhari kwa wadau wa sekta mbalimbali wanaotumia taarifa za hali ya hewa katika utekelezaji wa majukumu yao. Kwa kawaida, kipindi cha miezi ya Juni hadi Agosti (JJA), hutawaliwa na hali ya baridi na upepo mkali kwa maeneo mengi ya nchi. Kwa muhtasari, mwelekeo wa msimu wa JJA, 2025 unaonesha kuwa:
a)Mwelekeo wa hali ya joto
i.Hali ya baridi ya wastani hadi joto kiasi inatarajiwa katika maeneo mengi ya nchi. Hata hivyo, hali ya baridi ya wastani hadi baridi kali inatarajiwa katika maeneo ya mikoa ya Kigoma, Tabora, Katavi, Rukwa, Singida pamoja na maeneo ya magharibi mwa mkoa wa Dodoma.
ii.Vipindi vya baridi zaidi vinatarajiwa kujitokeza katika mwezi Julai.
iii.Vipindi vya mvua za nje ya msimu vinatarajiwa katika maeneo ya ukanda wa Ziwa Victoria, ukanda wa mwambao wa pwani pamoja na visiwa vya Unguja na Pemba.
b)Mwelekeo wa hali ya upepo
i. Msimu wa Kipupwe 2025 unatarajiwa kutawaliwa na upepo wa wastani utakaovuma kutoka Kusini Mashariki kwa maeneo mengi ya nchi, na vipindi vichache vya upepo mkali utakaovuma kutoka kusini (upepo wa kusi) hususan katika kipindi cha miezi ya Juni na Julai 2025 katika maeneo ya ukanda wa pwani ya Bahari ya Hindi na maeneo ya nchi kavu.
c)Athari
i. Magonjwa yanayohusiana na hali ya hewa ya baridi kama vile homa ya mapafu na magonjwa ya mifugo yanaweza kujitokeza, ingawa kwa kiasi kidogo.
ii.Hali ya vumbi linalosababishwa na upepo katika baadhi ya maeneo linaweza kupelekea uwepo wa magonjwa ya macho.