Machapisho

MWELEKEO WA MVUA ZA MSIMU WA MASIKA MACHI – MEI, 2025

Pakua

Dondoo muhimu za mvua za Masika (Machi – May), 2025

Taarifa hii inatoa uchambuzi wa mwenendo wa mifumo ya hali ya hewa na mwelekeo wa mvua za Masika kwa maeneo yanayopata misimu miwili ya mvua kwa mwaka (kanda ya Ziwa Victoria, nyanda za juu kaskazini mashariki, pwani ya kaskazini pamoja na maeneo yaliyopo kaskazini mwa mkoa wa Kigoma) katika kipindi cha miezi ya Machi hadi Mei, 2025. Ushauri na tahadhari umetolewa kwa wadau wa sekta mbalimbali wanaotumia taarifa za hali ya hewa katika utekelezaji wa majukumu yao kama vile kilimo na usalama wa chakula, mifugo na uvuvi, maliasili, wanyamapori na utalii, nishati na maji, usafirishaji (nchi kavu, kwenye maji na angani), mamlaka za miji, afya, sekta binafsi pamoja na menejimenti za maafa. Muhtasari wa mwelekeo wa mvua hizo na athari zake ni kama ifuatavyo:

a) Mwelekeo wa mvua za Masika kwa maeneo yanayopata misimu miwili ya mvua kwa mwaka:

i. Mvua za Wastani hadi Chini ya Wastani zinatarajiwa katika maeneo ya pwani ya kaskazini, kaskazini mwa mkoa wa Kigoma na ukanda wa Ziwa Victoria (Mikoa ya Kagera, Geita, Mwanza, Shinyanga na magharibi mwa mikoa ya Simiyu na Mara). Aidha, Mvua za Wastani hadi Juu ya Wastani zinatarajiwa katika maeneo mengi ya nyanda za juu kaskazini mashariki pamoja na mashariki mwa mikoa ya Mara na Simiyu.

ii. Mvua za Masika zinatarajiwa kuanza wiki ya kwanza na ya pili ya mwezi Machi , 2025 katika maeneo ya kanda ya Ziwa Victoria na pwani ya kaskazini; na katika wiki ya pili na ya tatu ya mwezi Machi, 2025 katika maeneo ya nyanda za juu kaskazini mashariki.

iii. Ongezeko la mvua linatarajiwa mwezi Aprili, 2025

b) Athari zinazotarajiwa:

i. Vipindi vya unyevu wa kuzidi kiasi pamoja na mafuriko vinaweza kujitokeza na kuathiri ukuaji wa mazao hususan katika maeneo yanayotarajiwa kupata mvua za Wastani hadi Juu ya Wastani.

ii. Kina cha maji katika mito na mabwawa kinatarajiwa kuongezeka hivyo kuongeza hatari ya mafuriko hususan katika maeneo yanayoathiriwa na mafuriko.

iii. Magonjwa ya mlipuko yanaweza kujitokeza kutokana na uchafuzi wa maji.

Kwa taarifa zaidi tafadhali pakua