Machapisho

MWELEKEO WA MVUA ZA MSIMU (NOVEMBA, 2024 - APRIL, 2025)

Pakua

Dondoo muhimu za mvua za Msimu (Novemba, 2024 – Aprili, 2025)

Taarifa hii inatoa uchambuzi wa mwenendo wa mifumo ya hali ya hewa na mwelekeo wa mvua za Msimu kwa maeneo yanayopata msimu mmoja wa mvua kwa mwaka (kanda ya magharibi, kati, nyanda za juu kusini magharibi, kusini mwa nchi, ukanda wa pwani ya kusini pamoja na maeneo yaliyopo kusini mwa mkoa wa Morogoro) katika kipindi cha miezi ya Novemba, 2024 hadi Aprili, 2025. Ushauri na tahadhari umetolewa kwa wadau wa sekta mbalimbali wanaotumia taarifa za hali ya hewa katika utekelezaji wa majukumu yao kama vile kilimo na usalama wa chakula, mifugo na uvuvi, maliasili, wanyamapori na utalii, nishati na maji, usafirishaji (nchi kavu, kwenye maji na angani), mamlaka za miji, afya, sekta binafsi pamoja na menejimenti za maafa. Muhtasari wa mwelekeo wa mvua hizo na athari zake ni kama ifuatavyo:

a) Mwelekeo wa mvua za Msimu kwa maeneo yanayopata msimu mmoja wa mvua kwa mwaka:

(i) Mvua za Wastani hadi Chini ya Wastani zinatarajiwa katika maeneo ya mikoa ya Kigoma, Tabora, Katavi, Rukwa, Songwe, Singida na Dodoma; kaskazini na mashariki mwa mkoa wa Lindi, na kaskazini mwa mikoa ya Mbeya na Iringa. Aidha, mvua za Wastani hadi Juu ya wastani zinatarajiwa katika mikoa ya Njombe, Ruvuma, Mtwara, maeneo ya kusini na magharibi mwa mkoa wa Lindi, kusini mwa mikoa ya Mbeya, Iringa na Morogoro.

(ii) Mvua zinatarajiwa kuanza wiki ya nne ya mwezi Oktoba, 2024 katika mkoa wa Kigoma na kusambaa katika maeneo mengine yanayopata mvua za Msimu mwezi Novemba, 2024 na mwisho katika mkoa wa Ruvuma Disemba, 2024.

(iii) Kipindi cha nusu ya pili ya msimu (Februari – Aprili, 2025) kinatarajiwa kuwa na mvua nyingi ikilinganishwa na nusu ya kwanza (Novemba, 2024 – Januari, 2025).

b) Athari na ushauri

(i) Shughuli za kilimo zinatarajiwa kuendelea kama ilivyo kawaida katika maeneo mengi katika mvua za Msimu 2024/2025. Hata hivyo, vipindi vya unyevu wa kuzidi kiasi pamoja na mafuriko vinaweza kujitokeza na kuathiri ukuaji wa mazao na miundombinu ya kilimo, hususan katika maeneo yanayotarajiwa kupata mvua za Wastani hadi Juu ya Wastani.

(ii) Kina cha maji katika mito na mabwawa kinatarajiwa kuongezeka, hali inayoweza kusababisha mafuriko, hasa katika maeneo yanayoathiriwa na mafuriko.

(iii) Jamii zinazokaa katika maeneo yenye hatari ya mafuriko zinashauriwa kuchukua hatua stahiki.