Machapisho

MWELEKEO WA HALI YA HEWA KWA KIPINDI CHA JUNI – AGOSTI (JJA), 2024

Pakua

Dondoo muhimu za hali ya hewa kipindi cha Juni-Agosti (JJA), 2024

Taarifa hii inatoa uchambuzi wa mwenendo wa mifumo ya hali ya hewa na mwelekeo wa hali ya joto, upepo na mvua katika msimu wa Juni hadi Agosti (JJA), 2024; Ushauri na tahadhari kwa wadau wa sekta mbalimbali wanaotumia taarifa za hali ya hewa katika utekelezaji wa majukumu yao. Kwa kawaida, kipindi cha miezi ya Juni hadi Agosti (JJA), hutawaliwa na hali ya baridi na upepo mkali kwa maeneo mengi ya nchi. Kwa muhtasari, mwelekeo wa msimu wa JJA, 2024 unaonesha kuwa:
a) Mwelekeo wa hali ya joto
i. Hali ya baridi ya wastani hadi joto kiasi inatarajiwa katika maeneo mengi ya nchi. Hata hivyo, hali ya baridi ya wastani hadi baridi kali inatarajiwa katika maeneo ya nyanda za juu kusini-magharibi na yale ya kusini mwa nchi.
ii. Vipindi vya baridi zaidi vinatarajiwa kujitokeza mwezi Julai.
b) Mwelekeo wa hali ya upepo
i. Msimu wa Kipupwe 2024 unatarajiwa kutawaliwa na upepo wa wastani hadi upepo mkali utakaovuma kutoka kusini-mashariki katika maeneo mengi na vipindi vichache vya upepo wa kusi katika ukanda wa pwani ya bahari ya Hindi na maeneo ya nchi kavu.
c) Mwelekeo wa mvua
i. Vipindi vya mvua vinatarajiwa katika baadhi ya maeneo ya ukanda wa pwani, nyanda za juu kaskazini mashariki na ukanda wa Ziwa Victoria pamoja na kaskazini mwa mkoa wa Kigoma.
d) Athari
i. Magonjwa yanayohusiana na hali ya hewa ya baridi kama vile homa ya mapafu na magonjwa ya mifugo yanaweza kujitokeza, ingawa kwa kiasi kidogo.
ii. Hali ya vumbi linalosababishwa na upepo katika baadhi ya maeneo linaweza kupelekea uwepo wa magonjwa ya macho.