Machapisho
MWELEKEO WA MVUA ZA MSIMU (NOVEMBA, 2023 – APRILI, 2024)
PakuaDondoo muhimu za mvua za Msimu (Novemba, 2023 – Aprili, 2024)
Taarifa hii inatoa uchambuzi wa mwenendo wa mifumo ya hali ya hewa na mwelekeo wa mvua za Msimu kwa maeneo yanayopata msimu mmoja wa mvua kwa mwaka (kanda ya magharibi, kati, nyanda za juu kusini magharibi, kusini mwa nchi, ukanda wa pwani ya kusini pamoja na maeneo yaliyopo kusini mwa mkoa wa Morogoro) katika kipindi cha miezi ya Novemba, 2023 hadi Aprili, 2024. Ushauri na tahadhari umetolewa kwa wadau wa sekta mbalimbali wanaotumia taarifa za hali ya hewa katika utekelezaji wa majukumu yao kama vile kilimo na usalama wa chakula, mifugo na uvuvi, maliasili, wanyamapori na utalii, nishati na maji, usafirishaji (nchi kavu, kwenye maji na angani), mamlaka za miji, afya, sekta binafsi pamoja na menejimenti za maafa. Muhtasari wa mwelekeo wa mvua hizo na athari zake ni kama ifuatavyo:
a) Mwelekeo wa mvua za Msimu kwa maeneo yanayopata msimu mmoja wa mvua kwa mwaka:
(i) Mvua za Juu ya Wastani hadi Wastani zinatarajiwa katika maeneo ya kusini mwa mkoa wa Morogoro, mikoa ya Iringa, Lindi, Mtwara, Singida, Dodoma, kaskazini mwa mkoa wa Katavi, Kigoma na Tabora. Aidha, mvua za Wastani hadi Juu ya Wastani zinatarajiwa kusini mwa mkoa wa Katavi, mikoa ya Njombe, Rukwa, Songwe, Mbeya na Ruvuma.
(ii) Mvua zinatarajiwa kuanza wiki ya nne ya mwezi Oktoba, 2023 katika maeneo ya magharibi na kutawanyika katika maeneo mengine mwezi Novemba, 2023.
(iii) Kipindi cha nusu ya kwanza ya msimu (Novemba, 2023 – Januari, 2024) kinatarajiwa kuwa na mvua nyingi ikilinganishwa na nusu ya pili (Februari – Aprili, 2024).
(iv) Uwepo wa El-Niño unatarajiwa kuwa na mchango mkubwa katika mvua za Msimu.
b) Athari na ushauri
(i) Shughuli za kilimo zinatarajiwa kuendelea kama ilivyo kawaida katika maeneo mengi. Hata hivyo, vipindi vya unyevu wa kuzidi kiasi pamoja na mafuriko vinaweza kujitokeza na kuathiri ukuaji wa mazao na miundombinu ya kilimo.
(ii) Kina cha maji katika mito na mabwawa kinatarajiwa kuongezeka.
(iii) Wadau mbalimbali wanashauriwa kuzingatia matumizi endelevu na uhifadhi wa rasilimali maji.