Machapisho
Taarifa ya Hali Mbaya ya Hewa kwa Mwezi Juni 2023
PakuaKatika kipindi cha mwezi Juni, 2023 hali ya ukavu, baridi ya wastani hadi baridi kali ilijitokeza katika maeneo mengi nchini na kusababisha upungufu wa unyevu ardhini, kupungua kwa maji na malisho pamoja na kuwepo kwa hali vumbi. Aidha, hali ya hewa iliyojitokeza pamoja na athari zake inaendana na taarifa ya mwelekeo wa msimu wa Kipupwe (Juni-Agosti), 2023 iliyotolewa mwezi Mei, 2023. Hata hivyo, katika wiki ya nne ya Juni, 2023 vipindi vya upepo mkali pia vilijitokeza na kuathiri baadhi ya maeneo ya ukanda wa pwani, kati mwa nchi na nyanda za juu kusini magharibi. Ingawa hali ya ukavu ilijitokeza katika maeneo mengi ya nchi lakini matukio machache ya mvua kubwa yalionekana katika maeneo ya pwani ya kaskazini, ukanda wa Ziwa Victoria na nyanda za juu kaskazini mashariki.