Machapisho

MWELEKEO WA MSIMU WA MVUA ZA MACHI – MEI, 2023 (MASIKA)

Pakua

Dondoo muhimu za msimu wa mvua za Masika; Machi - Mei 2023
Taarifa hii inatoa uchambuzi wa mwenendo wa mifumo ya hali ya hewa na mwelekeo wa msimu wa mvua za Masika katika kipindi cha Machi – Mei, 2023, ushauri kwa wadau wa sekta na mamlaka mbalimbali kama vile Kilimo na Usalama wa Chakula, Mifugo na Uvuvi, Utalii na Wanyamapori, Uchukuzi, Mamlaka za miji, Nishati, Maji na Madini, Afya pamoja na Menejimenti za Maafa. Baadhi ya mambo muhimu katika taarifa hii ni: -

i. Mvua za wastani hadi chini ya wastani zinatarajiwa katika maeneo mengi ya nchi yanayopata misimu miwili ya mvua kwa mwaka isipokuwa maeneo machache ya mikoa ya Dar es salaam, Pwani (ikijumuisha Mafia), kaskazini mwa Morogoro pamoja na kisiwa cha Unguja ambapo mvua za wastani hadi juu ya wastani zinatarajiwa.
ii. Ongezeko la mvua linatarajiwa katika kipindi cha mwezi Mei 2023, hususan katika maeneo ya pwani ya kaskazini.
iii. Mvua za Masika zinatarajiwa kuanza mwezi Machi, katika maeneo mengi na zinatarajiwa kuisha katika wiki ya nne ya mwezi Mei 2023 katika maeneo mengi ingawa mwendelezo wa mvua za nje ya msimu unatarajiwa mwezi Juni 2023 katika maeneo machache ya ukanda wa pwani ya kaskazini.

Athari zinazotarajiwa:


i. Mvua chache na zenye mtawanyiko usioridhisha katika maeneo yanayotarajiwa kupata mvua za wastani hadi chini ya wastani zinaweza kusababisha upungufu wa unyevu kwenye udongo na upatikanaji wa maji kwa ajili ya shughuli za kilimo.
ii. Katika maeneo yanayotarajiwa kupata mvua za wastani hadi juu ya wastani, unyevu wa udongo kupita kiasi unaweza kujitokeza na hivyo kuathiri ukuaji wa mazao ambayo hayahitaji maji mengi.
iii. Kwa kuwa maeneo mengi yanatarajiwa kupata mvua za wastani hadi chini ya wastani, viwango vya maji katika mito na mabwawa havitarajiwi kuathirika zaidi.