Machapisho

UTABIRI WA MVUA ZA MSIMU (NOVEMBA, 2022 – APRILI, 2023)

Pakua

Dondoo muhimu za mvua za Msimu (Novemba, 2022 – Aprili, 2023)

Taarifa hii inatoa uchambuzi wa mwenendo wa mifumo ya hali ya hewa na mwelekeo wa mvua za Msimu kwa maeneo yanayopata msimu mmoja wa mvua kwa mwaka (kanda ya magharibi, kati, nyanda za juu kusini magharibi, kusini mwa nchi, ukanda wa pwani ya kusini pamoja na maeneo yaliyopo kusini mwa mkoa wa Morogoro) katika kipindi cha miezi ya Novemba, 2022 hadi Aprili, 2023. Ushauri na tahadhari umetolewa kwa wadau wa sekta mbalimbali wanaotumia taarifa za hali ya hewa katika utekelezaji wa majukumu yao kama vile kilimo na usalama wa chakula, mifugo na uvuvi, maliasili, wanyamapori na utalii, nishati na maji, usafirishaji (nchi kavu, kwenye maji na angani), mamlaka za miji, afya, sekta binafsi pamoja na menejimenti za maafa. Muhtasari wa mwelekeo wa mvua hizo na athari zake ni kama ifuatavyo:

a) Mwelekeo wa mvua za Msimu kwa maeneo yanayopata msimu mmoja wa mvua kwa mwaka:

(i)Mvua za chini ya wastani hadi wastani zinatarajiwa katika maeneo mengi ya mikoa ya Kigoma, Tabora, Katavi, Singida, Dodoma, Ruvuma, Lindi na Mtwara. Aidha, mvua za wastani hadi chini ya wastani zinatarajiwa katika baadhi ya maeneo ya mikoa ya Njombe, Rukwa, Songwe, Mbeya, Iringa na kusini mwa mkoa wa Morogoro.

(ii)Katika nusu ya kwanza ya msimu (Novemba, 2022 – Januari, 2023) vipindi virefu vya ukavu vinatarajiwa kujitokeza.

(iii)Ongezeko la mvua linatarajiwa katika nusu ya pili ya msimu (Februari- Aprili, 2023). Aidha, mvua za nje ya msimu zinatarajiwa mwezi Mei, 2023 katika maeneo mengi.

(iv)Maeneo ya mikoa ya Singida na Dodoma mvua za Msimuzinatarajiwa kuanzakwa kuchelewa katika wiki ya pili ya mwezi Januari, 2023.

b) Athari na ushauri

(i)Katika kipindi cha Novemba na Disemba, 2022, upungufu mkubwa wa unyevunyevu katika udongo unatarajiwa kujitokeza katika maeneo mengi yanayopata mvua za Msimu na kuathiri ukuaji wa mazao na upatikanaji wa malisho kwa ajili ya mifugo.

(ii)Kina cha maji katika mito na mabwawa kinatarajiwa kupungua na kuathiri upatikanaji wa maji kwa matumizi mbalimbali kama vile umwagiliaji na uzalishaji wa nishati.

(iii)Mamlaka zinashauriwa kuhakikisha vyanzo vya maji vinatunzwa pamoja na kuweka miundombinu ya uvunaji maji sambamba na kuandaa na kutekeleza mipango mkakati ya kuhimiza kilimo himilivu.