Machapisho

MWELEKEO WA MSIMU WA MVUA ZA OKTOBA – DISEMBA, 2022 (VULI)

Pakua

Dondoo muhimu za msimu wa mvua za Vuli kipindi cha Oktoba – Disemba, 2022

Taarifa hii inatoa uchambuzi wa mwenendo wa mifumo ya hali ya hewa na mwelekeo wa msimu wa mvua za Vuli kipindi cha Oktoba - Disemba 2022, ushauri na tahadhari kwa wadau wa sekta mbalimbali kama vile kilimo na usalama wa chakula, mifugo na uvuvi, maliasili, wanyamapori na utalii, nishati na maji, usafirishaji (nchi kavu, kwenye maji na angani), mamlaka za miji, afya pamoja na menejimenti za maafa. Utabiri huu ni mahsusi kwa maeneo yanayopata misimu miwili ya mvua kwa mwaka (Nyanda za juu kaskazini mashariki, Pwani ya kaskazini, Ukanda wa Ziwa Viktoria pamoja na kaskazini mwa mkoa wa Kigoma). Kwa muhtasari, mwelekeo huo na athari zake unaonesha kuwa:

a)Mvua za Vuli, 2022

  • Mvua za Vuli zinatarajiwa kuwa za Chini ya Wastani hadi Wastani. Mvua hizo zinatarajiwa kuanza kwa kuchelewa, zenye mtawanyiko usioridhisha na kuambatana na vipindi virefu vya ukavu.
  • Mvua za Vuli zinatarajiwa kuanza wiki ya nne ya mwezi Septemba, 2022 katika ukanda wa Ziwa Victoria. Hata hivyo, katika maeneo ya nyanda za juu kaskazini mashariki na pwani ya kaskazini mvua zinatarajiwa kuanza kati ya wiki ya nne ya mwezi Oktoba na wiki ya kwanza ya mwezi Novemba, 2022.
  • Vipindi vya joto kali kuliko kawaida vinatarajiwa katika msimu wa Vuli hususani katika maeneo ya pwani ya kaskazini na nyanda za juu kaskazini mashariki.

b)Athari zinazotarajiwa

  • Upungufu wa unyevunyevu katika udongo unatarajiwa kujitokeza katika maeneo mengi.
  • Upungufu wa maji safi na salama unaweza kujitokeza na kuweza kuchochea magonjwa ya mlipuko.
  • Upungufu wa malisho na maji unaweza kujitokeza hivyo kupelekea migogoro kati ya wafugaji na watumiaji wengine wa ardhi.
  • Kina cha maji katika mito na mabwawa kinatarajiwa kupungua hivyo kunaweza kupelekea upungufu wa maji kwa matumizi mbalimbali.