Machapisho
MWELEKEO WA HALI YA HEWA KWA KIPINDI CHA JUNI – AGOSTI (JJA), 2022
PakuaDondoo muhimu za hali ya hewa kipindi cha Juni-Agosti (JJA), 2022
Taarifa hii inatoa uchambuzi wa mwenendo wa mifumo ya hali ya hewa pamoja na hali ya hewa inayotarajiwa katika msimu wa Kipupwe katika kipindi cha Juni hadi Agosti (JJA), 2022; Ushauri na tahadhari kwa wadau wa sekta mbalimbali wanaotumia taarifa za hali ya hewa katika utekelezaji wa majukumu yao. Kwa kawaida, kipindi cha miezi ya Juni hadi Agosti (JJA), huwa ni kipindi cha baridi na upepo kwa maeneo mengi ya nchi. Kwa muhtasari, mwelekeo huo kwa mwaka 2022 pamoja na athari zake unaonesha kuwa:
a)Viwango vya joto
- Katika kipindi cha JJA, 2022 hali ya baridi ya wastani hadi joto kiasi inatarajiwa katika maeneo mengi ya nchi. Hata hivyo, hali ya joto kiasi hadi baridi ya wastani inatarajiwa katika maeneo ya ukanda wa pwani ya kaskazini pamoja na nyanda za juu kaskazini mashariki.
- Vipindi vya baridi zaidi vinatarajiwa kujitokeza mwezi Juni na Julai.
- Vipindi vya baridi kali vinatarajiwa katika maeneo ya miinuko ya nyanda za juu kusini magharibi hususan nyakati za usiku na asubuhi.
b)Upepo
Katika kipindi cha miezi ya Juni na Agosti, 2022 vipindi vya upepo mkali vinatarajiwa kushamiri katika maeneo mengi nchini. Msimu wa Juni hadi Agosti 2022 unatarajiwa kuwa na upepo utakaovuma kutoka kusini-mashariki na mashariki (Matlai) katika ukanda wa pwani ya bahari ya Hindi na maeneo ya nchi kavu hususan mwezi Agosti, 2022.
c)Athari
- Magonjwa ya mifugo yanayoambatana na baridi kama vile homa ya mapafu yanaweza kujitokeza
- Hali ya vumbi inayoambatana na upepo mkali katika baadhi ya maeneo inatarajiwa kujitokeza na inaweza kuathiri afya ya binadamu na wanyama