Habari

Imewekwa: May, 17 2024

WAZIRI WA UCHUKUZI ASHIRIKI MKUTANO WA SITA WA MAWAZIRI WENYE DHAMANA YA MASUALA YA HALI YA HEWA BARANI AFRIKAAMCOMET

WAZIRI WA UCHUKUZI ASHIRIKI MKUTANO WA SITA WA MAWAZIRI WENYE DHAMANA YA MASUALA YA HALI YA HEWA BARANI AFRIKAAMCOMET

Dodoma, Tarehe 16 Mei 2024.

Tanzania kupitia Wizara ya Uchukuzi ikiongozwa na Waziri wa Uchukuzi, Mhe. Prof. Makame Mnyaa Mbarawa (Mb) na Wataalamu kutoka Wizara ya Uchukuzi na Mamlaka ya Hali ya Hewa Tanzania (TMA) walishiriki katika Mkutano wa Sita wa Baraza la Mawaziri wenye Dhamana ya Hali ya Hewa Barani Afrika (Sixth African Ministerial Conference on Meteorology – AMCOMET-6) uliofanyika tarehe 16 Mei 2024 kwa njia ya mtandao.

Mkutano huo wa AMCOMET ulipokea na kujadili taarifa ya utekelezaji wa shughuli za AMCOMET kutoka kwa Sekretarieti hiyo na kuridhia Mpango Mkakati wa utekelezaji wa masuala ya hali ya hewa Barani Afrika uliohuishwa pamoja na kuidhinisha Mpango wa Utafutaji Rasilimali kwa ajili ya utekelezaji wa Mkakati wa kuimarisha huduma za hali ya hewa Barani Afrika. Masuala mengine yaliyojitokeza tangu Mkutano wa Tano wa AMCOMET ulioofanyika Machi 2021, yalijadiliwa na kutolewa maazimio. Aidha, AMCOMET-6 imejadili maendeleo ya Sekta ya Hali ya Hewa na umuhimu wake kwa maendeleo ya kijamii na kiuchumi barani Afrika.

Vilevile wajumbe walijadili na kukubaliana umuhimu wa kuendelea kuzijengea uwezo wa kisera na kitaalamu Taasisi za Hali ya Hewa ili kuendelea kuimarisha ubora na ufanisi katika utoaji wa huduma hususan taarifa za utabiri na tahadhari za matukio ya hali mbaya ya hewa yanayochagizwa na mabadiliko ya hali ya hewa na tabianchi. Madhara yatokanayo na matukio ya hali mbaya ya hewa yameendelea kujitokeza kwa sura tofauti ikiwa ni pamoja na matukio ya mafuriko na ukame yanayoshuhudiwa Barani Afrika na kwa hivi karibuni katika eneo la Afrika Mashariki ikiwemo Tanzania. Huduma zinazotolewa na Taasisi za Hali ya Hewa ni sehemu ya utekelezaji wa Mpango wa Umoja wa Mataifa wa kuhakikisha kuwa, kila nchi inakuwa na mfumo mzuri wa utoaji wa tahadhari kwa watu wote ifikapo mwaka 2027 (UN Early Warning for All-AW4ALL initiative).

Akichangia katika mada ya Mkutano inayohusiana na maandalizi ya Mpango wa Utekelezaji, Ufuatiliaji na Tathmini na Mpango wa Kukusanya Rasilimali, Mhe. Prof. Mbarawa alimpongeza Mwenyekiti wa AMCOMET aliyemaliza muda wake (Cameroon) pamoja na Sekretarieti kwa kufanikisha maandalizi ya mipango hiyo, ambayo ni utekelezaji wa Mkakati Jumuishi wa Masuala ya Hali ya Hewa wa Afrika uliohuishwa (African Integrated Strategy on Meteorology) ambao Baraza la Mawaziri wa Umoja wa Afrika (AU) na Mkutano Mkuu wa Wakuu wa Nchi Wanachama wa AU waliupitisha mwaka 2022. “Haya ni mafanikio makubwa ya kisera ambayo sote tunapaswa kuhusika katika utekelezaji wake, hivyo tunapongeza sana kazi kubwa iliyofanywa hadi sasa. Hata hivyo ni vyema kuhakikisha kuwa mipango hii inaendana vyema na mipango mingine ya kikanda na kitaifa ili kuhakikisha kwamba hakuna anayeachwa nyuma katika utekelezaji wake” Alisema Prof. Mbarawa.

Baraza la Mawaziri wenye dhamana ya masuala ya hali ya hewa katika Bara la Afrika (AMCOMET) hukutana kila baada ya miaka miwili. Wajumbe wa mkutano wa AMCOMET ni Waheshimiwa Mawaziri wenye dhamana ya masuala ya hali ya hewa Barani Afrika na Mwenyekiti aliyepokea kijiti cha kuongoza AMCOMET kwa kipindi cha miaka miwili ijayo kuanzia 2024 hadi 2026 ni nchi ya Uganda.