Habari

Imewekwa: Oct, 14 2025

​WADAU WAHIMIZWA KUTUMIA TAARIFA ZA UTABIRI ZA MAENEO MADOGO MADOGO

​WADAU WAHIMIZWA KUTUMIA TAARIFA ZA UTABIRI ZA MAENEO MADOGO MADOGO

Dodoma,Tarehe 13 Oktoba 2025.

Mamlaka ya Hali ya Hewa Tanzania (TMA) imeendelea kukutana na wadau ikiwa ni mwendelezo wa ushirikishwaji wa wadau hususan wataalam kutoka sekta mbalimbali za kijamii na kiuchumi kwa lengo la kujadiliana kuhusu utabiri wa Msimu kwa kipindi cha mwezi Novemba, 2025 – Aprili, 2026.

Akifungua warsha hiyo, mgeni rasmi na Mwenyekiti wa Bodi TMA, Mhe. Jaji Mshibe Ali Bakari alitoa wito kwa wadau kufuatilia na kutumia taarifa za utabiri ili kuongeza tija katika shughuli za kiuchumi na kijamii. Warsha hiyo ilifanyika katika ukumbi wa PSSSF, jijini Dodoma, tarehe 13 Oktoba, 2025.

“Mamlaka imeendelea kuboresha huduma zake kwa utoaji wa taarifa za hali ya hewa kwa maeneo madogo madogo (Downscaled forecast), ikiwemo katika ngazi ya Wilaya. Hivyo, natoa wito kwa wadau wote tutumie vizuri tarifa hizi za utabiri zilizoboreshwa ili kuongeza tija na ufanisi katika shughuli zetu na kuimarisha mchango wa sekta ya hali ya hewa katika ukuaji wa uchumi..” Alisema Jaji Mshibe.

Naye, Kaimu Mkurugenzi Mkuu wa TMA na Makamu Mwenyekiti wa Jopo la Kimataifa la Sayansi ya Mabadiliko ya Hali ya Hewa na Tabianchi (IPCC), Dkt. Ladislaus Chang’a amesisitiza kuwa jitihada na ushirikiano mkubwa baina ya taasisi na wadau wote zinahitajika ili kujenga ustahimilivu wa jamii na taasisi mbalimbali za kitaifa katika kukabiliana na changamoto za mabadiliko ya hali ya hewa na tabianchi.

Katika hatua nyingine Dkt. Chang’a ameishukuru taasisi ya NORGES VEL ambayo imedhamini sehemu ya maandalizi na ufanikishaji wa mkutano huo kwani ushirikiano huo unaendelea kuimarisha uhusiano wa kimkakati kati ya TMA na wadau wa maendeleo katika kuhakikisha jamii inanufaika zaidi na huduma za hali ya hewa.

Naye, mwakilishi kutoka ofisi ya Waziri Mkuu, Mratibu wa Maafa, Bi. Consolata Mbanga alielezea namna taarifa za mapema za hali ya hewa zinavyosaidia katika kukabiliana na athari za matukio ya halu mbaya ya hewa. Ofisi ya Waziri Mkuu hutumia taarifa hizo kuandaa mpango wa kukabiliana na athari tarajiwa na kufuatilia mkoa kwa mkoa athari zinazojitokeza na kusaidia kukabiliana na athari hizo.