Habari

Imewekwa: Oct, 27 2021

TMA YATOA TUZO KWA WANAHABARI BORA WA TAARIFA ZA HALI YA HEWA 2021.

TMA YATOA TUZO KWA WANAHABARI BORA WA TAARIFA ZA HALI YA HEWA 2021.

Dar es Salaam, Tarehe 26/10/2021

Mamlaka ya Hali ya Hewa Tanzania (TMA) imetoa tuzo kwa wanahabari bora wa taarifa za hali ya hewa 2021, tuzo hizo zimetolewa kwa wanahabari waliofanya vizuri katika kutoa taarifa za hali ya hewa kwa jamii kwa kipindi cha mwaka mmoja kuanzia Septemba 2020 hadi Julai 2021 katika ukumbi wa mikutano wa Baraza la Wakunga na Wauguzi Tanzania – Kibaha.

Tuzo hizo zilitolewa rasmi na Mwenyekiti wa Bodi ya TMA, Dkt. Buruhani S. Nyenzi katika warsha ya wanahabari inayohusu mwelekeo wa mvua za msimu kwa kipindi cha mwezi Novemba 2021 hadi Aprili 2022, ambaye aliwapongeza washindi wa tuzo hizo na kuwapa hamasa wengine kuendelea kufanya kazi hizo kwa weledi ili ziweze kutambuliwa na Mamlaka na kuwa sehemu ya mchakato wa Tuzo hizo katika wakati ujao.

“Napenda kutumia nafasi hii kuwapongeza sana na kuwapa hamasa wengine kuendelea kufanya kazi bora zaidi na kuwasilisha taarifa za kazi zenu ili ziweze kutambuliwa na Mamlaka na kuwa sehemu ya mchakato wa tuzo hizo katika wakati ujao”. Alizungumza Dkt. Nyenzi.

Awali wakati wa ufunguzi wa warsha hiyo, Mkurugenzi Mkuu wa Mamlaka ya Hali ya Hewa Tanzania (TMA) ambaye pia ni Makamu wa Tatu wa Rais wa Shirika la Hali ya Hewa Duniani (WMO), Dkt. Agnes Kijazi alieleza kuwa kwa kipindi kirefu sasa TMA imeendelea kuandaa warsha kwa wanahabari kila inapokaribia kutoa utabiri wa msimu wa mvua, na aliahidi kuendeleza utaratibu huo ili kuhakikisha taarifa za hali ya hewa zinawafikia walengwa kwa usahihi na kwa wakati.

Utabiri wa msimu wa mvua za Vuli 2021 unatarajiwa kutolewa rasmi Tarehe 27/10/2021, katika ukumbi wa mikutano wa TMA, Ghorofa ya tatu, Ubungo Plaza, Dar es Salaam.