Habari
VIONGOZI NA WATAALAMU WA HALI YA HEWA WA ZIMBABWE WAANZA ZIARA YA MAFUNZO YA SIKU TANO NCHINI TANZANIA

Dar es Salaam; Tarehe 20 Mei 2025;
Viongozi waandamizi na wataalamu wa Idara ya Hali ya Hewa Zimbabwe (Meteorological Services Department (MSD)) wameanza ziara ya mafunzo ya siku tano nchini Tanzania kuanzia tarehe 19 hadi 23 Mei 2025 ili kujifunza na kujenga uwezo na umahiri katika masuala mbalimbali ya hali ya hewa katika ofisi za Mamlaka ya Hali ya Hewa Tanzania (TMA) zilizopo Ubungo Plaza, Dar Es Salaam, nchini Tanzania.
Akiwasilisha salamu za ukaribisho, Kaimu Mkurugenzi Mkuu wa TMA, na Makamu Mwenyekiti wa IPCC, Dkt. Ladislaus Chang’a aliushukuru uongozi wa MSD Zimbabwe kwa kuichagua TMA nchini Tanzania kati ya nchi zote Afrika ili kuja kufanya ziara ya mafunzo kwa lengo la kuboresha utendaji kazi katika taasisi yao.
‘Ni fursa nzuri ya kubadilishana uzoefu na kuimarishana katika jukumu letu la msingi la kutoa huduma za hali ya hewa kwa ajili ya kulinda maisha ya watu na mali zao. Kwa upande wetu TMA tupo tayari kutoa uzoefu wetu wa kiutendaji na kuwajengea uwezo wataalamu wa hali ya hewa wa Zimbabwe ikiwemo katika Mifumo ya Udhibiti wa Ubora, Mifumo ya Utabiri wa Hali ya Hewa, Uchakataji na utunzaji wa tarifa za hali ya hewa, Uangazi wa Hali ya Hewa, na utoaji wa Huduma za Hali ya Hewa kwa sekta mbalimbali’. Alisisitiza Dkt. Chang’a
Aidha, kwa upande wa Mkurugenzi wa MSD - Zimbabwe, Bi. Rebecca Manzou, akiwasilisha salamu kutoka Zimbabwe, aliishukuru TMA kwa ukaribisho na mapokezi mazuri wakiwa na matumaini makubwa ya kujifunza namna TMA ilivyopiga hatua katika sekta ya hali ya hewa ikiwemo kuimarisha uchakataji na utunzaji wa takwimu za hali ya hewa na matumizi ya teknolojia za kisasa katika huduma za hali ya hewa.