Habari

Imewekwa: Jan, 13 2023

TAARIFA KWA UMMA: HALI YA MWENENDO WA MVUA ZINAZOENDELEA KWA BAADHI YA MAENEO NCHINI.

TAARIFA KWA UMMA: HALI YA MWENENDO WA MVUA ZINAZOENDELEA KWA BAADHI YA MAENEO NCHINI.

Dar es Salaam, 13 Januari, 2023:

Mamlaka ya Hali ya Hewa Tanzania (TMA) inatoa taarifa kuhusu mwenendo wa mvua zinazoendelea nchini.

Mvua zinazoendelea kunyesha katika baadhi ya maeneo hapa nchini zimesababishwa na kuimarika kwa Ukanda Mvua (ITCZ) hususani katika wiki ya pili ya mwezi Januari, 2023. Hali hii imesababisha ongezeko la mvua katika baadhi ya maeneo nchini. Hata hivyo, vipindi vifupi vya mvua kubwa vimejitokeza katika maeneo machache na kusababisha athari mbalimbali ikiwemo baadhi ya makazi kuzungukwa na maji pamoja na miundombinu ya usafirishaji kutopitika vizuri.

Aidha, msimu wa mvua wa Novemba, 2022 hadi Aprili, 2023 ulishaanza mwezi Disemba, 2022 na unaendelea kama ulivyotabiriwa katika maeneo mengi yanayopata msimu mmoja wa mvua kwa Mwaka. Vile vile, mvua za nje ya msimu zinazoendelea katika maeneo yanayopata misimu miwili ya mvua kwa mwaka zinatarajiwa kupungua mwishoni mwa wiki ya pili ya mwezi Januari, 2023.

Kwa taarifa hii wananchi wanashauriwa kuendelea kuzingatia taarifa na tahadhari za hali mbaya ya hewa zinazotolewa na Mamlaka ya Hali ya Hewa Tanzania sambamba na kutafuta, kupata na kufuata ushauri wa wataalam katika sekta husika ili kupunguza athari zinazotokana na hali mbaya ya hewa.

Imetolewa na:

Mamlaka ya Hali ya Hewa Tanzania