Habari

Imewekwa: Oct, 25 2025

MWENENDO WA KIMBUNGA “CHENGE” KATIKA ENEO LA KUSINI MAGHARIBI MWA BAHARI YA HINDI

MWENENDO WA KIMBUNGA “CHENGE” KATIKA ENEO LA KUSINI MAGHARIBI MWA BAHARI YA HINDI

Dar es Salaam, 25 Oktoba, 2025 Mchana:

Mamlaka ya Hali ya Hewa Tanzania (TMA) inaendelea kutoa taarifa ya mwenendo wa Kimbunga “CHENGE” katika Bahari ya Hindi, Kaskazini mwa Kisiwa cha Madagascar.

Kimbunga “CHENGE” kimeendelea kusalia baharini na kusogea kuelekea magharibi, huku kikipungua nguvu yake. Hadi asubuhi ya leo kilikuwa katika eneo la Bahari umbali wa takribani kilometa 1,280 Mashariki mwa pwani ya kisiwa cha Mafia.

Uchambuzi wa mifumo ya hali ya hewa unaonesha kuwa Kimbunga hicho kinatarajiwa kuendelea kusogea kuelekea Magharibi zaidi mwa Bahari ya Hindi ulipo ukanda wa pwani wa nchi yetu huku kikiendelea kupungua nguvu yake kadri kinavyosogea. Hali hiyo inatarajiwa kusababisha uwezekano mdogo wa ongezeko kidogo la kasi ya upepo na mawimbi makubwa ya Bahari kati ya tarehe 26 hadi 28 ya Mwezi Oktoba, 2025 kwa maeneo ya ukanda wa pwani ya nchi yetu. Vilevile, upo uwezekano mdogo wa vipindi vichache vya mvua kubwa kujitokeza hususani katika maeneo ya visiwa vya Unguja na Pemba pamoja na mikoa ya Morogoro, Pwani, Dar es salaam na Tanga na maeneo jirani katika kipindi hicho cha tarehe 26 na 28 ya Mwezi Oktoba 2025.

Mamlaka ya Hali ya Hewa Tanzania (TMA) inaendelea kufuatilia mwenendo wa kimbunga “CHENGE” na athari zake kwa mifumo ya hali ya hewa hapa nchini na itaendelea kutoa taarifa kila inapobidi.

USHAURI: Watumiaji wa Bahari na wananchi kwa ujumla wanashauriwa kuendelea kufuatilia na kuzingatia taarifa za utabiri kutoka Mamlaka ya Hali ya Hewa Tanzania pamoja na kupata ushauri na miongozo ya wataalam wa kisekta.