Habari
MWENENDO WA KIMBUNGA “HIDAYA” KATIKA BAHARI YA HINDI MASHARIKI MWA PWANI YA TANZANIA

Dar es Salaam, 03 Mei 2024 saa 9:00 Mchana:
Mamlaka ya Hali ya Hewa Tanzania (TMA) inaendelea kutoa taarifa ya mwenendo wa kimbunga “HIDAYA” kilichopo katika Bahari ya Hindi mashariki mwa pwani ya nchi yetu. Kimbunga “HIDAYA” kimeendelea kuimarika na kusogea kuelekea maeneo ya pwani ya nchi yetu ambapo hadi kufika saa tatu asubuhi ya tarehe 03 Mei 2024 kilikuwa umbali wa takriban Kilomita 342 Mashariki mwa pwani ya Mtwara. Katika kipindi hiki kimbunga HIDAYA kimeendelea kuimarika zaidi huku kasi ya upepo ikiongezeka hadi kufikia Kilomita 140 kwa saa.
Mwenendo wa mifumo ya hali ya hewa baharini inaonesha uwezekano wa Kimbunga “HIDAYA” kupungua nguvu kiasi kwa saa 12 zijazo huku kikiendelea kusogea karibu kabisa na pwani ya Tanzania. Kimbunga hiki kinatarajiwa kuendelea kuwepo hadi tarehe 05 mwezi Mei 2024 na kupungua nguvu baada ya tarehe 05 Mei 2024.
Uwepo wa kimbunga “HIDAYA” karibu na pwani ya nchi yetu unatarajiwa kutawala na kuathiri mifumo ya hali ya hewa hapa nchini ikiwa ni pamoja na kusababisha vipindi vya mvua kubwa na upepo mkali katika baadhi ya maeneo ya mikoa ya Mtwara, Lindi, Pwani (ikijumuisha visiwa vya Mafia), Dar es Salaam, Tanga, Morogoro, visiwa vya Unguja na Pemba na maeneo ya jirani. Vipindi vya mvua na upepo mkali unaozidi kilometa 40 kwa saa tayari vimeanza kujitokeza katika maeneo ya Lindi na Mtwara hadi kufikia saa 9 mchana wa leo. Pamoja na kupungua nguvu kwa Kimbunga HIDAYA mawingu yanayoambatana na kimbunga hicho yanatarajiwa kusababisha vipindi vya mvua kubwa na upepo mkali katika maeneo mengine ya ukanda wa pwani kuelekea tarehe 4 hadi 5 Mei 2024.
USHAURI: Wananchi katika maeneo tajwa na wote wanaojihusisha na shughuli mbalimbali baharini wanashauriwa kuchukua tahadhari kubwa na pia kuendelea kufuatilia na kuzingatia taarifa za utabiri na tahadhari kutoka Mamlaka ya Hali ya Hewa Tanzania pamoja na kupata ushauri na miongozo ya wataalam katika sekta husika ili kujikinga na athari zinazoweza kujitokeza.
Mamlaka ya Hali ya Hewa Tanzania (TMA) inaendelea kufuatilia mwenendo wa kimbunga “HIDAYA” na athari zake kwa mifumo ya hali ya hewa hapa nchini na itaendelea kutoa taarifa kila baada ya masaa matatu, na mara kwa mara kila inapobidi.
Imetolewa na:
Mamlaka ya Hali ya Hewa Tanzania.