Habari
MKUU WA MAKAPTENI ZANZIBAR AELEZEA MIPANGO YA SAFARI INAVYOTEGEMEA TAARIFA ZA HALI YA HEWA.

Zanzibar, Tarehe 25 Juni 2025:
Mkuu wa Makapteni Zanzibar, Kapteni Kadadi Hassan Shea, ameelezea namna taarifa za hali ya hewa zinavyowasaidia katika kupanga safari zao baharini na kuepukana na hasara zinazoweza kujitokeza.
Alizungumza hayo kupitia vyombo vya habari alipokuwa ametembelea banda la Mamlaka ya Hali ya Hewa Tanzania (TMA) lililokuwa katika maonesho ya Maadhimisho ya Siku ya Mabaharia Duniani yaliyofanyika katika viwanja vya Mnazi Mmoja, Zanzibar kuanzia Tarehe 22 hadi 25 Juni 2025.
"Taarifa za hali ya hewa zinatusaidia sana katika kufanya mipango ya safari zetu baharini ili kuepusha au kupunguza hasara zinazoweza kujitokeza, mfano kukiwa na utabiri wa uwepo wa upepo mkali huwa tunajipanga kwa kuchukua mizigo kidogo katika kukabiliana nao, na kama kuna utabiri wa uwepo wa mvua tunachukua maamuzi ya kupakia mizigo, kama vile saruji, kwenye makontena," alielezea Kapteni Shea.
Kaptain shea aliongezea kuwa maonesho haya yanawapa fursa Mabaharia kukutana na kufahamiana na taasisi mbalimbali ili kuunganisha nguvu ya pamoja katika kuihudumia jamii kwa usalama na faida zaidi.
Kwa upande wake Mkurugenzi wa TMA Ofisi ya Zanzibar, Ndg. Masoud Makame Faki, alisema ushiriki wa Mamlaka katika maonesho hayo yanajielezea kupitia kauli mbiu yake inayosema "Bahari Yetu, Wajibu Wetu na Fursa Yetu," ambapo kupitia kipengele cha wajibu wetu TMA inawajibika katika kuelezea namna huduma za hali ya hewa zinavyoweza kusaidia katika kuokoa maisha ya mabaharia, wasafiri na mali kwa ujumla.