Habari
KIPUPWE 2024: HALI YA BARIDI YA WASTANI HADI JOTO KIASI INATARAJIWA KATIKA MAENEO MENGI YA NCHI.
Dodoma; Tarehe 27 Mei, 2024;
Mamlaka ya Hali ya Hewa Tanzania (TMA) imeeleza kuwa maeneo mengi ya nchi yanatarajiwa kuwa na hali ya baridi ya wastani hadi joto kiasi katika msimu wa kipupwe 2024.
Hayo yalisemwa na Kaimu Mkurugenzi Mkuu wa TMA na Makamu Mwenyekiti wa Jopo la Sayansi ya Mabadiliko ya Hali ya Hewa na Tabianchi (IPCC), Dkt. Ladislaus Chang’a , wakati akitoa taarifa kwa umma kuhusu mwelekeo wa hali ya hewa kwa kipindi cha Juni – Agosti (JJA),2024 katika ofisi za makao makuu ya TMA, Dodoma.
“Katika kipindi cha msimu wa Kipupwe 2024, hali ya baridi ya wastani hadi joto kiasi inatarajiwa, hata hivyo, hali ya baridi zaidi inatarajiwa katika maeneo ya nyanda za juu kusini-magharibi (Mikoa ya Mbeya, Songwe, Iringa, Njombe pamoja na maeneo ya kusini mwa mkoa wa Morogoro). Msimu huu wa Kipupwe, 2024 unatarajiwa kuwa na upepo wa wastani hadi upepo mkali utakaovuma kutoka kusini-mashariki na vipindi vichache vya upepo wa kusi katika ukanda wa pwani ya bahari ya Hindi na maeneo ya nchi kavu. Kwa ujumla, upepo wa wastani unatarajiwa kushamiri katika maeneo mengine ya nchi.” Alisema Dkt. Chang’a.
Aidha, Dkt. chang’a aliongezea kwa kusema “licha ya hali ya ukavu inayotarajiwa katika maeneo mengi nchini katika kipindi hiki, kunatarajiwa kuwepo na vipindi vya mvua katika maeneo ya ukanda wa Ziwa Victoria (mikoa ya Kagera, Geita, Simiyu na Mara), kaskazini mwa mkoa wa Kigoma, nyanda za juu kaskazini-mashariki (mikoa ya Arusha na Kilimanjaro) pamoja na ukanda wa pwani (mikoa ya Dar es Salaam, Tanga, Morogoro, Mtwara, Lindi, Pwani ikijumuisha visiwa vya Mafia, pamoja na visiwa vya Unguja na Pemba”.
Kupitia taarifa yake Dkt. chang’a ameeleza pia athari zinazoweza kujitokeza pamoja na kutoa ushauri kwa wadau wa sekta mbalimbali wanaotumia taarifa za hali ya hewa katika kutekeleza majukumu yao ya kila siku. Akitolea mfano sekta ya Afya Dkt. Chang’a alisema “Magonjwa yanayohusiana na hali ya hewa ya baridi kama vile homa ya mapafu na magonjwa ya mifugo yanaweza kujitokeza, ingawa kwa kiasi kidogo. Pia vumbi linalosababishwa na upepo katika baadhi ya maeneo linaweza kupelekea uwepo wa magonjwa ya macho.”
Akimaliza kutoa taarifa hiyo, Dkt. Chang’a alisema, Mamlaka ya Hali ya Hewa Tanzania itaendelea kufuatilia mwenendo wa mifumo ya hali ya hewa na kutoa mirejesho kadri inavyohitajika hususani kipindi hiki cha mabadiliko ya hali ya hewa. Aidha, wadau wanashauriwa kuwasiliana na Mamlaka husika ili kupata taarifa za kisekta ili kukidhi mahitaji maalum katika sekta zao.