Seasional Forecast
Mwelekeo wa Mvua za Vuli (Oktoba - Desemba), 2026
Dondoo muhimu za msimu wa mvua za Vuli (Oktoba – Desemba), 2026
Taarifa hii inatoa uchambuzi wa mwenendo wa mifumo ya hali ya hewa na kutoa mwelekeo wa msimu wa mvua za Vuli (Oktoba hadi Desemba), 2026. Pia, inawasilisha ushauri na tahadhari za mapema kwa wadau wa sekta mbalimbali ambazo zimekuwa zikiathiriwa na mabadiliko ya hali ya hewa kama vile Kilimo na Usalama wa chakula, Mifugo na Uvuvi, Utalii na Wanyamapori, Usafiri na Usafirishaji (nchi kavu, kwenye maji na angani), Mamlaka za Miji, Sekta Binafsi, Vyombo vya Habari, Nishati, Ujenzi, Maji na Madini, Afya pamoja na Menejimenti za Maafa. Utabiri huu ni mahsusi kwa maeneo (Nyanda za juu kaskazini mashariki, Pwani ya kaskazini, Ukanda wa Ziwa Viktoria pamoja na kaskazini mwa mkoa wa Kigoma) yanayopata misimu miwili ya mvua kwa mwaka. Kwa muhtasari, mwelekeo huo na athari zake unaonesha kuwa:
a) Mvua za msimu wa Vuli, 2026
i.Msimu wa mvua za Vuli, 2026 unatarajiwa kuathiriwa kwa kiwango kikubwa na hali ya El Niño yenye nguvu kubwa.
ii.Mvua za Vuli, 2026 zinatarajiwa kuwa za Juu ya Wastani hadi Wastani katika maeneo mengi ya Ukanda wa Pwani ya Kaskazini, Nyanda za Juu Kaskazini Mashariki, Ukanda wa Ziwa Viktoria na kaskazini mwa Mkoa wa Kigoma.
iii.Mvua za Vuli, 2026 zinatarajiwa kuanza wiki ya nne ya mwezi Septemba na wiki ya kwanza ya mwezi Oktoba, 2026 katika maeneo ya ukanda wa Ziwa Viktoria na baadae kusambaa taratibu katika maeneo mengine mwezi Oktoba. Kwa kawaida, mvua za Vuli huisha mwezi Desemba; hata hivyo, katika msimu huu mvua za nje ya msimu zinatarajiwa kuendelea hadi mwezi Januari, 2027.
iv.Ongezeko la mvua linatarajiwa katika kipindi cha mwezi Novemba, 2026.
b) Athari zinazotarajiwa
i.Vipindi vya unyevu kwenye udongo wa kuzidi kiasi pamoja na mafuriko vinaweza kujitokeza na kuathiri ukuaji wa mazao na miundombinu ya kilimo. Hata hivyo, katika baadhi ya maeneo shughuli za kilimo zinatarajiwa kuendelea kama kawaida katika msimu huu wa Vuli, 2026.
ii.Ongezeko la kina cha maji katika mabwawa na mito linatarajiwa kujitokeza, hali ambayo inaweza kuathiri miundombinu ya rasilimali za maji na nishati.
iii.Magonjwa ya mlipuko yanaweza kujitokeza kutokana na uchafuzi wa maji.
Kwa taarifa zaidi tafadhali pakua

