Habari

Imewekwa: May, 24 2025

TMA NA CRDB YAWANOA MAAFISA UGANI MBEYA, NJOMBE, IRINGA NA SONGWE

TMA NA CRDB YAWANOA MAAFISA UGANI MBEYA, NJOMBE, IRINGA NA SONGWE

Wataalamu wa Mamlaka ya Hali ya Hewa (TMA) kwa kushirikiana na Benki ya CRDB kupitia mradi wa Tanzania Agriculture Climate Adaptation Technology Deployment Project (TACATDP) wamewajengea uwezo Maafisa Ugani wa namna bora ya kutafsiri na kutumia taarifa za hali ya hewa hususani katika shughuli za kilimo.

Akizungumza wakati wa kufungua mafunzo hayo Meneja wa Kanda ya Nyanda za Juu Kusini Magharibi (TMA) Bw. Elias Elipiki, alisema mafunzo hayo yanawalenga Maafisa Ugani kwani wao ni daraja kati ya TMA na wakulima, hivyo mafunzo haya yanalenga kutoa elimu ya namna sahihi ya kutafsiri taarifa za hali ya hewa zinazotolewa na Mamlaka na kuwawezesha wakulima kufanya mipango sahihi juu ya shughuli za kilimo kwa msimu husika.

Aidha, Meneja Uhusiano kutoka CRDB ambaye pia ni msimamizi wa utoaji wa mikopo inayozingatiwa uhifadhi wa mazingira katika mradi wa (TACATDP) Bw. Karim Kindole, alisema CRDB na TMA wana ushirikiano katika kuwajengea uwezo Maafisa Ugani namna ya kudhibiti na kuwasaidia wakulima kupata taarifa sahihi za mabadiliko ya hali ya hewa.

Naye, Afisa Kilimo kutoka Halmashauri ya Wilaya ya Mbarali Bw. Sostenesi Silayo, aliwashukuru TMA na CRDB kwa kuwapa nafasi Maafisa Ugani kupata elimu ambayo wataitumia katika kuwashauri wakulima kulima kilimo sahihi kutokana na hali ya hewa husika na kuongeza tija katika uzalishaji wa mazao mengi.